Kamishna wa Nishati Tanzania, Mhandisi Innocent Luoga, ameongoza Timu ya wataalam wa nishati, kupokea Rasimu ya Mpango unaolenga uainishaji wa mahitaji na matumizi ya gesi asilia katika makazi na viwanda vya ndani ya nchi.

Kamishna wa Nishati nchini, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) akipokea rasimu ya mpango wa uainishaji wa mahitaji na matumizi ya gesi katika makazi na viwanda vya ndani ya nchi, kutoka kwa mmoja wa wataalam kutoka JICA, Shinji Omoteyama, Juni 12, mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

Mhandisi Luoga alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua kupokea rasimu husika iliyowasilishwa na wataalam kutoka Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA), jana, Juni 12 mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

“Mpango huu umelenga kuainisha matumizi ya gesi majumbani, viwandani, usafiri pamoja na maeneo mengine mbalimbali ndani ya nchi,” alifafanua Mhandisi Luoga.

Alisema kuwa, baada ya kupokea taarifa hiyo ya awali, Serikali itaupitia na kutoa mapendekezo yake yanayolenga kuuboresha kabla ya kuanza kutekelezwa.

Akifafanua zaidi kuhusu Mpango husika; Luoga alieleza kuwa,Timu ya wataalam hao kutoka JICA, ilikwishafanya utafiti katika Mikoa Saba (7) nchini ambayo ndiyo itahusika katika utekelezaji wake. Mikoa hiyo ni Mwanza, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dodoma, Morogoro na Mbeya.

Alieleza kuwa, awali, Serikali kupitia JICA iliandaa Mpango wa kwanza wa matumizi ya gesi nchini ujulikanao kama NGUMP (Natural Gas Utilization Master Plan), ambao ulikamilika Desemba 2016.

“Mpango huo wa kwanza uliainisha matumizi ya gesi katika maeneo mbalimbali ambayo ni pamoja na uzalishaji umeme, matumizi ya majumbani, viwandani na kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.”

Kamishna wa Nishati nchini, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza-kushoto) na wataalam wa nishati, wakifuatilia uwasilishwaji wa Rasimu ya Mpango unaolenga uainishaji wa mahitaji na matumizi ya gesi asilia katika makazi na viwanda vya ndani ya nchi; uliofanywa na wataalam kutoka JICA (hawapo pichani), Juni 12 mwaka huu, Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma.

Alisema kuwa, baada ya kukamilika kwa Mpango huo wa kwanza, sasa JICA wanaendelea kuandaa Mpango huu mwingine kwa ajili ya kuanisha matumizi ya gesi majumbani na viwanda vya ndani ya nchi pekee.

JICA inaisaidia Tanzania kuandaa Mpango husika kama sehemu ya misaada yake inayotoa nchini.

Na Veronica Simba – Dodoma.