Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini, walioko Makao Makuu Dodoma, wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha sikukuu ya Mei Mosi.

Baadhi ya wafanyakazi bora wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini walioko Makao Makuu Dodoma, (walioshika vyeti) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wenzao, mara baada ya kukabidhiwa zawadi na vyeti rasmi wakati wa maadhimisho ya sherehe ya wafanyakazi (Mei Mosi).

Katika kuadhimisha sikukuu hiyo muhimu, wafanyakazi hao walishiriki maandamano yaliyoanzia katika viwanja vya bunge na kuhitimishwa katika uwanja wa Jamhuri, ambapo walipokewa na Mgeni Rasmi; Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge.

Pamoja na mambo mengine yaliyofanyika wakati wa sherehe hizo, wafanyakazi bora walipatiwa zawadi na vyeti vya kutambua mchango wao.

Baadhi ya Wafanyakazi bora kutoka Idara mbalimbali za Wizara ya Nishati ni Mwamvita Mkakile kutoka Idara ya Nishati, Margaret Vava (Utawala) na Vera Sikana (Sera na Mipango). Taratibu za kuwapata wafanyakazi bora wengine kutoka Idara zilizosalia zinakamilishwa ili waweze kupatiwa vyeti pamoja na zawadi zao.

Kwa upande wa Wizara ya Madini, wafanyakazi bora ni Happy Ndunguru kutoka Idara ya Utawala ambaye pia ndiye mfanyakazi bora wa Wizara. Wengine ni Eugenia Mashoko (Uhasibu), Godfrey Nyamsenda (Sheria), Zuwena Msuya (Mawasiliano Serikalini), Josephat Mbwambo (Sera na Mipango), Christopher Mwita (TEHAMA), Dorothy Mtweve (Madini), Eric Kwesigabo (Ugavi) na Hassan Ngwandu (Ukaguzi wa Ndani).

Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini waliopo Makao Makuu Dodoma, wakishiriki maandamano ya Mei Mosi, 2018.

Na Veronica Simba – Dodoma.