Zaidi ya Wateja 22,700 wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa usafirishaji wa umeme wa kilovolti 220 wa Makambako-Songea unaotarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2018 na kuwezesha umeme kusambazwa katika mikoa na wilaya zote za  Njombe na Ruvuma ikiwa ni pamoja na kusambaza umeme vijijini kwa umbali wa kilomita 900.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo na miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini awamu ya Tatu inayoendelea nchi nzima.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akikagua vifaa vilivyopo katika eneo linalojengwa kituo cha kupoza umeme cha Makambako.

Kalemani alianzia ziara yake ya kukagua mradi huo mjini Makambako katika kituo kikubwa cha kupoza umeme cha Makambako ambapo hakuridhishwa na kasi ya maendeleo ya ujenzi katika kituo hicho na kuagiza mkandarasi kufikisha vifaa vyote vinavyotakiwa ili ujenzi uendelee.

“Naagiza ujenzi uende kwa kasi na wafanyakazi waongezwe wafanye kazi usiku na mchana,” alisisitiza Kalemani.

Dkt. Kalemani ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuacha kuzalisha umeme wa mafuta katika wilaya ya Namtumbo, Tunduru, Nyasa pamoja na maeneo yote yanayopata huduma ya umeme unaozalishwa kwa kutumia mafuta.

Amesema matarajio ni makubwa na serikali inajipanga kusimamia kwa nguvu zote mradi huo ili ukamilike kwa muda uliopangwa.

Pia, Waziri Kalemani amemwagiza Meneja wa TANESCO Makambako kutoa taarifa ya maendeleo ya mradi kila siku ili kujiridhisha na maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

Aidha, alimuagiza  Mkuu wa Mkoa wa Njombe,  Christopher Ole Sendeka kuendelea kusaidia katika kusimamia mradi huo “na ikiwezekana vyombo vya Ulinzi na Usalama viwe hapa ili kusaidia mradi uwe salama na wafanyakazi kubaki kazini ili mradi ukamilike kwa haraka.

kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe,  Christopher Ole Sendeka alisema kuwa, atafuatilia utekelezaji wa mradi huo mara kwa mara ili  kuhakikisha kuwa maelekezo ya Serikali yanafanyika kwa wakati na kwa viwango vilivyowekwa.

“Hili ni jukumu langu, nitatimiza wajibu wangu kuhakikisha kwamba majukumu ya Serikali yanatekelezwa kwa wakati, na nitafuatilia vifaa vinavyohitajika kwenye mradi huu vinavyodaiwa kuwa vimeagizwa, “.alisema.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa tatu toka kulia) na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka (kushoto kwa Waziri) wakitembea kuelekea eneo lililosimikwa nguzo kwa ajili ya kuwekwa transfoma katika kituo cha kupoza umeme cha Makambako.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi wa Makambako Songea Mhandisi Emmanuel Anderson, alimuahidi Waziri wa Nishati kuwa ifikapo mwezi Agosti mwakani mradi utakuwa umekamilika kama makubaliano yalivyo.

Kwa upande wake,  Kaimu mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Pololet Mgema aliishukuru Serikali kwa juhudi kubwa wanazozichukua katika kuhakikisha umeme unawafikia watanzania wote.

Alisema kuwa, miradi ya umeme inayotekelezwa nchini ina manufaa makubwa kwani itawafungulia wananchi fursa ya kujiajiri kupitia shughuli mbalimbali zinazotegemea nishati hiyo.