Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuongeza kasi ya uunganishaji wa Gesi asilia kwa matumizi ya viwandani na majumbani ili ifikapo mwezi Novemba mwaka huu, kiwanda cha Coca-Cola Kwanza kianze kutumia Gesi hiyo Kama ilivyokusudiwa.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu (wa pili kushoto ) akionyeshwa sehemu ambayo utafungwa mtambo wa Gesi Asilia kwa ajili kiwanda cha kutengeneza vinywaji baridi cha Coca-Cola Kwanza, alipofanya ziara ya kukagua usambazaji na uunganishaji wa miundombinu ya Gesi Katika kiwanda hicho. Kushoto kwa Naibu waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo akifuatiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba.

Mgalu alitoa Kauli hiyo jijini Dar es salaam tarehe 17 Septemba, 2018 wakati wa ziara ya kukagua miundombinu ya usambazaji na uunganishaji wa Gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani, viwandani na katika magari.

Katika ziara hiyo Mgalu alitembelea kiwanda cha kutengeneza vinywaji baridi cha Coca-Cola Kwanza ambacho kinatarajia kuanza kutumia Gesi asilia badala ya mafuta ifikapo mwezi Novemba mwaka huu ili kuendesha mashine mbalimbali zinazotumika katika uzalishaji wa bidhaa zinazotengezwa na kiwanda hicho.

Akiwa kiwandani hapo, aliwaagiza watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuharakisha ukamilishaji wa miundombinu ya kuzambaza Gesi kwa matumizi viwandani ili kuvipunguzia gharama ya uendeshaji viwanda vinavyotumia mafuta.

Sambamba na hilo aliwashauri wamiliki wa viwanda vyote nchini kuanza kutumia Gesi asilia badala ya mafuta kwa kuwa inapatikana kwa bei nafuu, pia wananchi wajiandae kwa kuweka miundombinu ya kuunganishwa na Gesi kwa matumizi ya nyumbani kwa kuwa itaanza kusambazwa hivi karibuni.

Aidha Mgalu alitembelea Kituo cha kujaza Gesi (Gas filling station) katika magari yanayotumia Gesi hiyo badala ya mafuta na kuzungumza baadhi ya madereva wa magari yaliyokuwa yakipata huduma hiyo kama inavyokuwa katika vituo vya kujaza mafuta.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati ) akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Dora Ernest (kushoto) wa TPDC, ya namna ambavyo miundombinu ya Gesi inavyounganishwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani.

Moja ya maombi yaliyotolewa na madereva hao ni Serikali kuweka vituo kama hivyo katika maeneo mbalimbali katika la Jiji la Dar es Salaam na mikoani kama vilivyo vituo vya kujaza mafuta ili waweze kupata huduma hiyo kwa urahisi tofauti na ilivyo sasa.

Hata hivyo, Naibu waziri Mgalu alipokea maombi hayo na kuahidi kuyafanyia kazi huku akiwashauri wamiliki wa magari kutumia Gesi asilia badala ya mafuta ili kupunguza gharama na kwa gesi ni rafiki wa mazingira.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makore wameipongeza Serikali kupitia wizara ya Nishati kwa kuona umuhimu wa kusambaza gesi kwa matumizi ya nyumbani, viwandani na kwenye magari kwa kuwa hatua hiyo itapunguza gharama ya maisha kwa wananchi.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, alimhakikishia Naibu Waziri Mgalu kuwa, Shirika hilo linafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kuwa huduma hiyo inawafikia wananchi kabla ya muda ili kumuwezesha kila Mtanzania kunufaika na rasilimali hiyo.

Mhandisi Kapuulya aliweka wazi kuwa karibu miundombinu yote iliyopangwa kujengwa kwa ajili ya kuwafikia wateja, yaani kaya zaidi ya 500 za awali kwa Jiji la Dar es Salaam katika maeneo ya Mwenge, Mlalakuwa, Mikocheni, pamoja na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam imekamilika.

Vilevile katika kiwanda cha Coca-Cola Kwanza miundombinu imekamilika ila kinachosubiriwa ni kifaa kimoja kilichoagizwa kutoka nchini India.

Katika ziara hiyo pia, Naibu waziri Mgalu alipata wasaa wa kuzungumza na mkandarasi, kampuni ya Nakuroi, anayetekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA III) katika mkoa wa Rukwa na Kagera na kumueleza kuwa ashirikiane na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa vifaa vinavyotumika katika ujenzi wa miundombinu ya mradi REA vinakuwa na ubora unaotakiwa.

Na Zuena Msuya