Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani, ametoa onyo kwa watendaji mbalimbali wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), wanaoshindwa kuwaunganishia umeme wananchi waliolipia huduma hiyo, kwa kisingizio cha kutokuwa na nguzo.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kushoto), akimkabidhi Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde kifaa cha Umeme Tayari (UMETA), alipofanya ziara katika Kijiji cha Fufu wilayani Chamwino kukagua utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) pamoja na kuwasha umeme, Juni 17, 2018. Waziri alitoa vifaa vya UMETA 10 kama zawadi kwa wananchi wa eneo hilo.

Alitoa onyo hilo jana, Juni 17, 2018 katika Kijiji cha Fufu, wilayani Chamwino, Mkoa wa Dodoma, alipofanya ziara kukagua utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) sambamba na kuwasha umeme katika eneo hilo.

“Nakuagiza Kamishna wa Nishati, kuanzia leo, nisije nikasikia mtaalam au Meneja yeyote wa TANESCO nchi nzima, ameshindwa kuwaunganishia wateja umeme kwa kisingizio cha kutokuwa na nguzo. Tutaanza kuwawajibisha mara moja,” alisisitiza Waziri.

Waziri alitoa maelekezo kuwa ni kazi ya watendaji hao wa TANESCO kufanya utaratibu wa kuzifuata nguzo mahali zilipo na kwamba hilo siyo jukumu la wateja.

Aidha, aliwataka watendaji hao kuhakikisha kuwa wateja wote waliolipia umeme, wanaunganishiwa huduma hiyo ndani ya siku Saba.

Alifafanua kuwa, mtendaji yeyote atakayeshindwa kumuunganishia mteja aliyelipia umeme ndani ya siku Saba, itatafsiriwa kuwa amejipatia pesa kwa njia isiyo halali na atawajibishwa.

Akizungumzia faida za umeme wa REA, Waziri Kalemani aliwashauri wananchi wanaopitiwa na Mradi huo, kufanya jitihada za kuhakikisha wanaunganishiwa umeme huo wenye gharama nafuu, kabla ya Mradi kuisha.

“Kama bado unajenga nyumba yako, fanya mchakato utundikiwe umeme wa REA kabla Mradi haujaisha. Hii ni kwa sababu gharama za kuunganisha umeme wa REA ni nafuu sana, maana kwa kiasi kikubwa zinalipwa na Serikali,” alisisitiza.

Suala jingine ambalo Waziri alisisitiza ni kwa wananchi kutumia kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kinachowezesha kupata huduma ya umeme pasipo kutandaza nyaya kwenye jengo husika.

Kwa upande wa Kijiji cha Fufu, aliwaambia wananchi kuwa, Mkandarasi atawapatia bure vifaa hivyo wananchi 250 wa kwanza, watakaowahi kuunganishiwa umeme. Hata hivyo, alisema kuwa kwa wale watakaokosa awamu hiyo, watauziwa kwa bei ya Serikali ambayo ni shilingi 36,000 tu.

“Ole wake Mkandarasi atakayebainika kuviuza vifaa hivi, atachukuliwa hatua.”

Kamishna wa Nishati, Mhandisi Innocent Luoga akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) katika Kijiji cha Fufu wilayani Chamwino kukagua utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) pamoja na kuwasha umeme, Juni 17, 2018.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mtera, Livingstone Lusinde, pamoja na kumshukuru Waziri na Serikali kwa ujumla kwa kazi ya kuwapelekea wananchi umeme; alieleza kuwa zoezi hilo limekuwa na changamoto ya kuruka baadhi ya vijiji.

Akitoa majibu kwa Mbunge na wananchi kuhusu changamoto hiyo, Waziri Kalemani alitoa maagizo kwa wakandarasi wanaotekeleza Mradi husika nchi nzima, kuhakikisha hawaruki kijiji, kitongoji wala mtu yeyote.

Awali, akiwasilisha taarifa ya TANESCO Wilaya ya Chamwino, Meneja wa Wilaya wa Shirika hilo, Baltazar Massawe, alimweleza Waziri kuwa, Mradi wa REA III katika Wilaya yake unahusisha usambazaji wa umeme katika vijiji 37 na unatekelezwa na Mkandarasi A2Z Infra Engineering Limited.

Na Veronica Simba – Dodoma