Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amepongeza Wizara  ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa  kukamilisha Mradi wa Kuzalisha  Umeme kwa Kutumia Gesi Asilia wa Kinyerezi II uliopo jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipata maelezo toka kwa Waziri wa Nishati Dkt. Medard kalemani kabla ya kuzindua mradi huo.

Rais Magufuli aliyasema hayo  tarehe 03 Aprili mwaka huu kwenye uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi waandamizi  kutoka Wizara tofauti, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), wabunge, wakandarasi wa mradi, na mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini.

Alisema kuwa uzalendo na kasi kubwa ya utekelezaji wa mradi imepelekea kituo hicho kukamilika kabla ya wakati na kuongeza kuwa sasa wananchi wataanza kuona manufaa ya gesi iliyogundukiwa Mtwara.

“  Ule msemo wa Hapa Kazi Tu nimeuona ukitekelezwa kwa vitendo  na  Wizara  ya Nishati na Tanesco, napenda muendelee na kasi hii kutekeleza miradi mingine iliyobakia na kupelekea kufikisha Megawati 5000 ifikapo mwaka 2020” alisema Rais Magufuli.

Aliendelea kusema kuwa, katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa umeme wa uhakika nchini Serikali imebuni miradi mbalimbali ya umeme ikiwa ni pamoja na miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko  ya maji ya mto Rufiji wa Stieglers Gorge ambao mara baada ya kukamilika utaongeza Megawati  2100 kwenye  Gridi ya Taifa.

Aliitaka Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme nchini hususan katika maeneo ya vijijini ambayo asilimia kubwa ya wananchi wanaishi huko.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliitaka Wizara pamoja na Tanesco kuangalia namna ya kupunguza gharama za umeme mara baada ya umeme wa kutosha kupatikana.

Wakati huohuo akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alisema kuwa mradi wa Kinyerezi II- 240MW ulibuniwa ili kuongeza uwezo wa kufua umeme kutokana na gesi asilia na hivyo kuimarisha na kuongeza uwezo wa gridi ya Taifa katika kusafirisha na kusambaza umeme nchini ambapo mradi ukikamilika utaongeza jumla ya Megawati 240 kwenye gridi ya taifa.

Dkt. Kalemani alisema kituo hiki kilichojengwa na kampuni ya Sumitomo Corporation kutoka Japan kitatumia teknolojia mpya na ya kwanza kutumika nchini ambapo ina hatua mbili ya kufua umeme (Combined cycle).

Alisema gharama za mradi huu ulioanza kutekelezwa tarehe 1 Machi, 2016 ni Dola za Marekani milioni 344 sawa na takribani Shilingi bilioni 758.

“Gharama hizi hazihusishi kodi mbalimbali kama vile Gharama za njia ya reli na bandari, tozo ya mizigo mizito inayotozwa na TANROADS na VAT. Mpaka sasa gharama ya mradi imefikia Dola za Marekani milioni 356.2. Gharama hii inajumuisha kodi na tozo mbalimbali zilizokwishalipwa na TANESCO,” alifafanua Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani aliendelea kusema kuwa mradi huu unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa njia ya mkopo kutoka benki ya Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC) na Japan Bank for International Cooperation (JBIC) za Japani chini ya mpango wa mikopo ya masharti nafuu kwa asilimia 85% sawa na Dola za Marekani milioni 292.4 na pia mchango wa Serikali ya Tanzania kwa asilimia 15% sawa na Dola za Marekani milioni 51.60.

Waziri Kalemani alisisitiza kuwa Serikali imeshalipa fedha yote inayohitajika yaani asilimia 15% ya fedha za mradi kiasi cha Dola za Marekani milioni 51.60.

Aliendelea kusema kuwa, hadi kufikia mwisho wa mwezi Februari 2018 malipo ya kiasi cha Dola za Marekani milioni 258.8 kwa ajili ya kazi zinazoendelea yamekwishafanyika kutoka kwenye kiasi cha dola za Marekani milioni 292.4 (mkopo wa masharti nafuu wa 85%) ambayo ni sawa na asilimia 88.5.

Dkt. Kalemani alisema mradi huu ulihusisha  ununuzi, usanifu, utengenezaji wa mitambo na viambata vyake, usafirishaji wa mitambo, ujenzi na ufungaji wa mitambo, ujenzi wa miundombinu ya ndani na nje ya kituo (k.m. barabara n.k.), ujenzi wa kituo cha kupokea na kupozea umeme (substation) na hatimaye kukabidhiwa mitambo ya kufua umeme baada ya kazi zote kukamilika.

Awali akielezea  utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka alisema kuwa utekelezaji wa mradi umekamilika kwa asilimia 91.84 ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Agosti mwaka huu.

Aliongeza kuwa  tayari mitambo sita imeshaanza kufanya kazi na kuzalisha jumla ya Megawati 167.82 kwenye Gridi ya Taifa  na kuongeza kuwa kazi inayoendelea kwa sasa ni ujenzi na ufungaji  wa mitambo miwili inayotumia mvuke (steam turbines) kuzalisha umeme ambapo itaongeza uwezo wa Megawati 80.4 kwenye  Gridi ya Taifa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamis Mwinyimvua akieleza jambo katika uzinduzi huo.

Aliendelea kufafanua kuwa mtambo wa kwanza unaotumia mvuke wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 40.2 utawashwa mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.

Alifafanua kuwa kazi nyingine zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa nguzo za kupokelea laini ya msongo wa kilovolti 220kV Kinyerezi I hadi Kinyerezi II na misingi ya mitambo.

Naye mwakilishi wa Balozi wa Japan Nchini, Hiroyuki Kubota alishukuru kwa ushirikiano kutoka kwa wadau mbalimbali kutoka katika taasisi za serikali na binafsi katika kufanikisha ukamilishaji wa mradi kabla ya wakati na kusisitiza kuwa Serikali ya Japan itaendelea kushirikiana na Serikali ya  Tanzania katika miradi mbalimbali ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2025 nchi inaingia katika orodha ya nchi zenye kipato cha kati.

Kubota alisema kuwa, ili nchi  kuingia katika uchumi wa kati inategemea viwanda ambavyo  vinahitaji  nishati ya umeme wa uhakika na kusisitiza kuwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya  Tano, Japan ipo tayari kuleta teknolojia yake kwenye sekta ya  umeme na miundombinu ili kuboresha uchumi  wa  viwanda nchini.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam