Naibu Waziri wa Madini Subira Mgalu amesema kuwa Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa 6 ambayo wananchi wake walirukwa katika utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme Awamu ya II, hivyo, REA III itawafikia wateja hao.

Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo akimkaribisha Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (aliyekaa mwenye kilimba) mara tu baada ya kuwasili katika kijiji cha Balang’a Wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga. Wengine katika Picha ni baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Mgalu aliyasema hayo wakati wa ziara yake katika kijiji cha Balang’a na Gombero wilayani Kilindi mkoani mkoani humo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi huo mwishoni mwa wiki.

Alisema kuwa, kwa upande wa Tanga, mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Nemis Company Ltd na hivyo kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi huyo ili kuwezesha zoezi hilo kufanyika kwa muda mfupi.

Aidha, Naibu Waziri Mgalu alimtaka mkandarasi anayefanya kazi katika Wilaya ya Kilindi kuhakikisha kuwa ifikapo mwezi Machi mwaka huu Wananchi wa Balang’a wawe wameunganishwa na umeme na wale wa Gombero wawe wamefikiwa na nishati hiyo ifikapo mwezi Mei mwaka huu.

Pia, Mgalu aliwataka wananchi kujiandaa wakati mradi husika utakapofika katika maeneo yao watumie fursa ya nishati hiyo ili iweze kuwainua katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wananchi wa Kijiji Balang’a Wilayani Kilindi Mkoa wa Tanga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo alisema kuwa bado wilaya ya Kilindi haijafikiwa na nishati ya umeme kwa kiwango kikubwa japokuwa zipo juhudi ambazo zimefanyika kwa upande uwekaji miundombinu ya umeme na kuongeza kuwa, ni vijiji 21 tu ndivyo vilivyounganishwa na nishati hiyo wilayani humo katika miradi ya REA I na REA II.

Mtondoo aliongeza kuwa, pamoja na wananchi wengi kutounganishwa na umeme, wale waliounganishwa na nishati hiyo wanalalamikia suala la kukatikakatika kwa umeme. “Tunaomba serikali ilitazame suala hilo kwa jicho la karibu ili wananchi waendeshe shughuli zao za kiuchumi,” aliongeza Mtondoo.

Na Rhoda James, Kilindi.