Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, leo, Juni 19, 2018 ameongoza timu ya viongozi na wataalam mbalimbali wa Wizara, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), katika majadiliano na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD); ambao wameahidi kuanza utekelezaji wa Mradi mkubwa wa umeme jua hapa nchini, ifikapo Februari mwakani.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akiagana na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Remy Rioux; baada ya kikao baina yao kujadili utekelezaji wa miradi ya umeme nchini. Kikao kilifanyika Juni 19, 2018 Makao Makuu ya Wizara, Dodoma.

Ujumbe huo wa AFD umemweleza Waziri kuwa, wako katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu mbalimbali zinazotakiwa, zitakazowezesha utiaji saini Makubaliano ya Awali (MoU) kati yake na Serikali.

“Endapo mambo yatakwenda vema, Mradi husika utaanza ndani ya kipindi cha miezi Sita kutoka sasa,” alifafanua Mtendaji Mkuu wa AFD, Remy Rioux.

Imeelezwa kwamba, Mradi huo mkubwa utakaozalisha umeme wa megawati 150, utatekelezwa mkoani Shinyanga.

Sambamba na Mradi wa Umeme jua, imeelezwa kuwa AFD pia wako katika hatua za mwisho kukamilisha taratibu husika kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa megawati 87 katika eneo la Kakono mkoani Kagera.

Waziri Kalemani, pamoja na kuishukuru AFD kwa utayari wao kufadhili miradi hiyo mikubwa itakayowasaidia Watanzania, ameahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano kadri inavyotakiwa katika kuhakikisha miradi husika inatekelezwa kikamilifu.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (mwenye shati ya bluu-kulia), akizungumza, wakati wa kikao baina ya viongozi na wataalam wa Wizara, TANESCO, REA (kulia) na Ujumbe kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), ulioongozwa na Mtendaji wake Mkuu, Remy Rioux. Kikao hicho kilifanyika Juni 19, 2018 Makao Makuu ya Wizara, Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dkt. Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga ni miongoni mwa walioshiriki kikao hicho.

Na Veronica Simba – Dodoma