Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu, amesema Serikali haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayechelewesha miradi ya Nishati nchini.

Naibu waziri wa Nishati, subira Mgalu akiwasha rasmi umeme katika kijiji cha Ibaga shuleni katika Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA.

Mgalu alisema hayo wakati wa  ziara yake katika Wilaya ya Mkalama mkoani Singida ambapo aliwasha rasmi umeme katika kijiji cha Ibaga Shuleni, Ibaga center na Nkinto Ikurui pamoja na kukagua shughuli za utekelezaji wa mradi wa REA  II katika kijiji cha Nkinto Kinyantungu.

REA II wilayani Mkalama ilichelewa kukamilika kutokana na kampuni ya ukandarasi  ya Spencon aliyekuwa akitekeleza mradi huo kushindwa kufanya kazi hiyo kwa kiwango kinachotakiwa hivyo kuilazimu Serikali kusitisha mkataba wake na kuipatia kampuni nyingine ya ukandarasi ya JV Emec.

Katika vijiji hivyo jumla ya wateja 48 wamelipia huduma ya umeme, 30 kati yao wamekwishaunganishwa  , 18 wanaendelea kuunganishwa, lengo likiwa ni kuwafikia wanakijiji wote katika Wilaya hiyo watakaokidhi   viwango vya kuunganishwa na huduma hiyo.

Katika hatua nyingine, Mgalu aliwaagiza Mameneja wanaosimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA kutoa taarifa mapema endapo hawaridhishwi na kasi ya mkandarasi ili Serikali iweze kuchukua hatua za haraka.

Naibu waziri wa Nishati, subira Mgalu akikagua mashine ya kukamua mafuta ya alizeti baada ya ya huduma ya umeme kufika katika kijiji cha Ibaga center katika Wilaya ya Mkalama mkoani Singida, alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa REA.

Aliongeza kuwa,  Serikali haitamvumilia meneja yeyote atakayeshindwa kusimamia majukumu yake ikiwemo kumsimamia mkandarasi  anayetekeleza Miradi ya REA.

Alisema kuwa, usimamizi wenye kuleta matokeo chanya ndiyo itakuwa kipimo cha utendaji kazi wa mameneja hao katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuunganisha vijiji vyote nchini na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2021.

“Mameneja ninyi ndiyo mnakuwepo maeneno ya mradi wakati wote, mnafahamu kasi ya utendaji kazi wa mkandarasi na viwango, mkiona kama mkandarasi anasuasua hawezi kazi toeni taarifa mapema ili kazi hiyo apewe mwingine, Hatutakubali kurudi nyuma, wananchi wanahitaji huduma ya umeme na fedha za kutekeleza hilo zipo”, Alisisitiza Mgalu .

Aliagiza kuwa wakandarasi wote wahakikishe kuwa wanakuwa na yadi za vifaa na miundombunu mbalimbali ya umeme  ili kurahisisha  utekelezaji wa mradi husika.

Na Zuena Msuya