Imeelezwa kuwa Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), inatekeleza jumla ya miradi 56 yenye thamani ya shilingi bilioni 4.7 inayolenga kuboresha miundombinu na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Machi 18 mwaka huu, walipotembelea Kituo hicho wakiwa katika ziara ya kazi mkoani humo.

Hayo yameelezwa Machi 18 mwaka huu na Meneja wa TANESCO Mkoa wa Singida Mhandisi Abdulrahman Nyenye, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakati wa ziara yake kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme mkoani humo.

“Pia tumejipanga kusogeza huduma karibu zaidi na wateja kwa kuwafuata walipo ambapo mpaka sasa tuna ofisi ndogo tano za Itigi, Mitundu, Ikungi, Ndago na Shelui na tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya umeme na athari zake,” alieleza.

Mhandisi Nyeye alieleza kuwa, Mkoa wa Singida unapata umeme kutoka Gridi ya Taifa kupitia njia kuu za kusafirishia umeme za msongo wa kilovoti 220 na 400. Aidha aliongeza kuwa Mkoa huo una kituo kikubwa kimoja cha kupooza umeme cha Kibaoni chenye uwezo wa wa MVA 40.

Akielezea idadi ya wateja katika Mkoa huo, alisema kuwa jumla yao ni 33,180 ambapo wateja wadogo ni 33,149 na wateja wa kati wapo 30, wakati mteja mkubwa ni mmoja.

Aidha, alibainisha kuwa mahitaji ya juu ya umeme kwa Mkoa ni megawati 9.4.

Vilevile, Mhandisi Nyenye aliieleza Kamati ya Bunge kuwa, Mkoa wa Singida umebahatika kupata miradi ya umeme vijijini (REA) kwa awamu zote tatu, ambapo awamu ya kwanza vijiji 22 vilipatiwa umeme na wateja 1,455 waliunganishwa.

“Katika Mradi wa REA awamu ya pili, vijiji 35 vilipatiwa umeme ambapo jumla ya wateja 2,836 waliunganishwa kati ya wateja 8,648 waliotarajiwa kupewa umeme,” alisema.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa Mradi huo haukukamilika kutokana na Mkandarasi M/S Spencon Services Limited aliyepewa kazi hiyo kushindwa kuikamilisha kwa wakati na hivyo kusitishiwa mkataba wake na Serikali.

Msimamizi wa Kituo cha Kupozea Umeme Singida, Mhandisi Malili Lucas akionesha namna kituo hicho kinavyofanya kazi kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Machi 18 mwaka huu. Kamati hiyo ilikuwa katika ziara ya kazi mkoani humo.

Kuhusu mradi wa REA awamu ya tatu, alisema kuwa matarajio ni kuwaunganisha wateja 11, 251 katika vijiji 150 ambapo gharama yake inakadiriwa kuwa shilingi 29,555,217,177.38 na Dola 5,338,879.92.

Alisema kuwa, Mkoa wa Singida pia ulibahatika kuwa miongoni mwa Mikoa iliyopata mradi wa laini kubwa ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 670 kutoka Iringa kupitia Dodoma na Singida hadi kwenye kituo cha kupooza umeme cha Ibadakuli Shinyanga. “Tayari mradi huo umekamilika,” alieleza.

Mkoa wa Singida una Wilaya Nne za ki-TANESCO ambazo ni Singida, Manyoni, Mkalama na Kiomboi.

Na Veronica Simba – Singida