Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, amesema kuwa, baada ya miezi mitatu Serikali itatoa uamuzi kama nchi iendelee kutumia mita za umeme zinazotengenezwa nje ya nchi au kupiga marufuku uingizaji wa mita hizo baada ya kujiridhisha  na uwezo wa viwanda vya ndani katika kuzalisha  mita husika.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kulia) akipata maelezo kuhusu uzalishaji wa mita za umeme katika kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme nchini. Wengine katika picha ni watendaji wa kiwanda hicho, Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Hashim Ibrahim na wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.

Dkt. Kalemani ameyasema hayo  jijini Dar es Salam tarehe 23 Machi, 2018 wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme lengo likiwa ni kujiridhisha na uwezo wa kiwanda hicho katika kukidhi mahitaji ya mita nchini.

“Serikali imeweka miezi mitatu ya matazamio ili kuona kama viwanda  vyetu ambavyo sasa ni viwili, vina uwezo wa kuzalisha mita za umeme  za kutosha na zenye ubora zitakazokidhi soko la ndani kisha tutatoa uamuzi kuhusu uingizaji wa mita hizo nchini,” alisema Dkt. Kalemani.

” Miezi kadhaa iliyopita Serikali ilitoa katazo la kuagiza nguzo za umeme na transfoma kutoka nje ya nchi, baada ya kujiridhisha kuwa uwezo wa kuzalisha vifaa hivyo tunao. Sasa katika mita hizi za umeme pia tunafanya ukaguzi ili kujiridhisha na uwezo wetu,” aliongeza  Dkt Kalemani.

Alisema kuwa, uzalishaji wa vifaa vya umeme nchini una faida mbalimbali ikiwemo kupungua kwa gharama za usafirishaji, mita kupatikana kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa wingi.

” Mfano gharama ya  mita moja ya njia moja ya umeme (single phase) kutoka nje ya nchi ni shilingi 150,000 na njia Tatu za umeme (three phase)  ni mpaka shilingi Laki Saba lakini mita zinazozalishwa nchini unazipata si kwa zaidi ya shilingi 120,000 kwa mita za njia moja ya umeme na haizidi shilingi  Laki Nne na Nusu kwa mita za njia Tatu za umeme,” alisema.

Awali Mkurugenzi wa kiwanda hicho cha Baobab, Hashim Ibrahim, alimweleza Dkt Kalemani  kuwa kiwanda hicho kina unawezo wa kuzalisha mita 38,000 kwa mwezi na kwa mwaka wanazalisha mita 456,000.

Aliongeza kuwa, mita hizo zina faida mbalimbali ikiwemo kuwa na mfumo wenye uwezo wa kuzuia matukio ya wizi wa umeme kwa asilimia 99 na kudhibiti upotevu wa umeme.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa kwanza kulia) akizungumza na watendaji wa Kiwanda cha Baobab Energy Systems kinachozalisha mita za umeme nchini . Katikati ni Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Hashim Ibrahim.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, ambaye ni Meneja Mwandamizi wa Mauzo na Masoko wa Shirika hilo, Theodory Bayona, alisema kuwa mahitaji ya Shirika hilo ni mita 20,000 kwa mwezi ambapo kati ya hizo, takriban mita 1000 ni za njia tatu za umeme. Kiasi hicho cha mita ni kwa ajili ya wateja wapya.

Aliongeza kuwa, mahitaji ya mita za umeme bado ni makubwa kwani kuna miradi ya usambazaji umeme bado inaendelea nchini na pia kazi ya ubadilishaji wa mita za zamani bado inaendelea.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazalishaji wa vifaa vya umeme nchini kuzalisha vifaa vyenye ubora pamoja na kutoviuza vifaa hivyo kwa gharama ya juu kwani vinazalishwa hapahapa nchini.

Na Teresia Mhagama