Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, amesema, Serikali imejiridhisha pasipo shaka, kuwa wazalishaji wa ndani wa vifaa vya umeme wana uwezo mkubwa unaotosheleza mahitaji ya nchi na ziada.

Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, akizungumza wakati wa kikao baina ya Uongozi wa Wizara na Wazalishaji pamoja na Wagavi wa vifaa vya umeme, wanaotekeleza Mradi wa REA III (hawapo pichani), katika kikao kazi kilichofanyika Juni 28, mwaka huu, katika Ukumbi wa Chuo cha VETA Dodoma. Katikati ni Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Haji Janabi.

Kwa sababu hiyo, Waziri amewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi mbalimbali ya umeme nchini, hususan Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu (REA III), kuachana na visingizio kwamba wanalazimika kuagiza vifaa hivyo nje ya nchi.

Msimamo huo wa Serikali, unakuja kufuatia kikao baina ya Uongozi wa Wizara na Wakandarasi, Wazalishaji pamoja na Wagavi wa vifaa vya umeme, wanaotekeleza Mradi wa REA III; uliofanyika Juni 28, mwaka huu, katika Ukumbi wa Chuo cha VETA Dodoma.

“Mimi na viongozi wenzangu tumefarijika sana kuthibitisha kuwa wazalishaji wa ndani ya nchi, wana uwezo wa kuzalisha vifaa vya kutosha zaidi hata ya mahitaji yaliyopo kwa sasa.”

Katika kikao hicho, Waziri Kalemani aliwaagiza wakandarasi husika kuhakikisha wanaainisha mahitaji yao ya vifaa na kuyawasilisha mapema kwa wazalishaji, ili kuwe na muda wa kutosha wa kuviandaa na hivyo wavipate kwa wakati stahiki. Aliwaagiza kutekeleza agizo hilo kwa kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Julai.

“Tukumbuke kwamba, viwanda vyetu vya ndani bado ni vichanga. Ukimtaka mzalishaji akupe nguzo 500 ndani ya siku chache, ni kutaka kumkwamisha. Anahitaji muda wa kutosha kuweza kukutengenezea vifaa hivyo kwa ubora unaotakiwa; hivyo toeni oda zenu mapema,” alisisitiza Waziri.

Aidha, Dkt. Kalemani aliwataka wazalishaji, wakandarasi na wataalam wa REA na TANESCO kufanya kazi kwa ushirikiano ili malengo ya Serikali kuwapelekea wananchi wake umeme wa kutosha na kwa wakati, yatimie.

Vilevile, Waziri alisisitiza kuhusu matumizi ya lugha nzuri kwa wananchi ambako miradi ya umeme vijijini inatekelezwa. Alisema kuwa, kumekuwepo na tabia ya baadhi ya wakandarasi kutumia lugha kali na ya kuudhi kwa wananchi, hivyo aliwataka kuacha mara moja.

Katika hatua nyingine, Waziri alitoa agizo kwa kila Mkandarasi kuhakikisha anatoa vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) kwa Taasisi zote za Umma zilizopo katika eneo lake la Mradi, ili kuzipunguzia gharama. “Tunataka tutengeneze mazingira mepesi kwa wateja wetu.”

Pia, aliwataka kuhakikisha wanatekeleza kazi zao katika kila eneo linalowahusu kwa wakati mmoja, badala ya kufanya hivyo katika baadhi tu ya maeneo huku wananchi wa maeneo mengine wakisubiri kwa muda mrefu kufikiwa na huduma.

Wadau mbalimbali wakichangia hoja wakati wa kikao kazi baina ya Uongozi wa Wizara ya Nishati, Wazalishaji pamoja na Wagavi wa vifaa vya umeme, wanaotekeleza Mradi wa REA III kilichofanyika Juni 28, mwaka huu, katika Ukumbi wa Chuo cha VETA Dodoma.

Hata hivyo, Waziri aliwapongeza wadau hao wote kwa utendaji kazi mzuri na kwa ushirikiano ambao wamekuwa wakiuonesha kwa Serikali. Aliwataka kuendeleza ushirikiano huo na kuwaahidi kuwa, kwa upande wake, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano stahiki kwa wadau hao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, pamoja na kuunga mkono pongezi zilizotolewa na Waziri kwa wadau husika; aliwataka kuongeza bidii zaidi katika kazi hiyo ili kuunganisha umeme katika vijiji vingi zaidi.

“Nami pia nimejiridhisha pasipo shaka kuwa uwezo wa ndani kuzalisha vifaa upo. Niwaombe tu, tuendeleze ushirikiano na tuwashe vijiji vingi zaidi.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara Haji Janabi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Kahitwa Bishaija na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga, waliahidi kusimamia utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Viongozi wa Wizara.

Na Veronica Simba – Dodoma.