Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amewaagiza Wenyeviti wa Vijiji nchini kote, ambako miradi ya umeme vijijini inatekelezwa, kuwasimamia wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ili wakamilishe kazi kwa wakati.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani akiwasha umeme katika Jengo la Kituo cha Afya cha Rondo, Lindi Vijijini, Septemba 27, 2018 kuashiria uwashaji rasmi wau meme katika eneo hilo. Wanaoshuhudia tukio hilo ni viongozi mbalimbali wa Serikali na wananchi wakiongozwa na Mbunge na Waziri Mstaafu Benard Membe.

Alitoa maagizo hayo kwa nyakati tofauti Septemba 27 mwaka huu, akiwa katika ziara ya kazi katika vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Lindi ambako aliwasha rasmi umeme na kuzungumza na wananchi.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia) akimkabidhi kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Sarah Chiwamba (kushoto), wakati wa hafla ya kuwasha rasmi umeme katika eneo hilo. Tukio hilo lilifanyika Septemba 27, 2018.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Katika kuhakikisha maagizo yake yanatekelezwa, Waziri Kalemani aliwataka wakandarasi kuripoti kila siku asubuhi kwa wenyeviti wa vijiji husika, ambako wanatekeleza miradi ili kujiridhisha kuwa wapo kazini.

Aidha, Waziri aliwataka wenyeviti hao kujiridhisha kuwa wakandarasi husika hawaajiri vibarua kutoka nje ya maeneo yao bali watoke katika vijiji husika. “Mwenyekiti ukigundua kuwa Mkandarasi kaajiri vibarua kutoka nje, mtaarifu Mkuu wa Wilaya mara moja ili achukue hatua stahiki.”

Vilevile, aliwaagiza Mameneja wa TANESCO wa Kanda na Wilaya kuongeza nguvu katika zoezi hilo la kuwasimamia wakandarasi ili kuhakikisha wanafanya kazi ipasavyo.

Akiwa mkoani Lindi, Waziri kalemani aliwasha umeme katika vijiji vya Chipande (Lindi Vijijini), Luchelegwa (Luangwa) na Legezamwendo (Liwale).

Na Veronica Simba