Imeelezwa kuwa, shilingi bilioni 21 zimetengwa katika Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi waliopisha mradi mkubwa wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 utakaoanzia Kinyerezi kuelekea Chalinze, Segera, Tanga na Dodoma.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza jambo mbele ya wananchi waliofika kujua hatma ya malipo yao ya fidia ya kupisha mradi wa kusafirisha umeme wa kV 400 katika Kata ya Kinyerezi jijini Dar Es Salaam.

Hayo yamebainishwa tarehe 21 Februari, 2018 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu katika mkutano uliohudhuriwa na Mbunge wa Jimbo  la Segerea, Bona Karua na wananchi wa kata ya Kinyerezi walioachia maeneo yao ili kupisha ujenzi wa njia hiyo ya umeme.

Mgalu alisema kuwa, fedha za kuwalipa fidia wananchi hao zipo na kwa sasa zinasubiri kukamilika kwa taratibu mbalimbali ili wananchi waweze kulipwa na kueleza kuwa mradi hautaweza kuanza kabla ya fidia hizo kutolewa.

Alisisitiza kuwa, mikubwa ya nishati haitaanza kutekelezwa mpaka Serikali itakapokamilisha kuwalipa wananchi fidia zao na hivyo kurahisisha ujenzi wa miradi hiyo.

Akizungumzia umuhimu wa mradi huo kwa Taifa, Mgalu alisema kuwa, ujenzi wa Reli ya kisasa kutoka Dar es salaam kuelekea Dodoma kufanikiwa kwake kunategemea kukamilika kwa njia hiyo ya umeme ili uweze kutumika katika kuendesha treni hiyo ya kisasa itakayotumia umeme mwingi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,  Khalid James alisema tathmini imekwishafanyika na majina ya wanaostahili kulipwa yamewasilishwa kwa  kamati iliyoundwa ili kuhakiki endapo majina yaliyowasilishwa ni sahihi ili kupata uhakika wa kufanya malipo hayo kwa watu sahihi.

Baadhi ya wananchi waliofika ili kuwasilisha malalamiko ya madai ya fidia ya kupisha mradi wa njia ya umeme katika kata ya Kinyerezi kwa Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.

Aidha aliongeza kuwa, uwepo wa watendaji wachache wasiokuwa waaminifu wanaoingiza majina yasiyo sahihi kumepelekea taratibu za malipo kuchukua muda mrefu na alisisitiza kuwa fedha haitatolewa mpaka Serikali itakapojiridhisha na idadi ya wanaostahili kulipwa pamoja na kiasi cha fedha wanachopaswa kulipwa.

Naibu Waziri Mgalu alitembelea pia, kata ya Kifuru na Kibaga jijini Dar es Salaam ili kujionea maeneo inakotarajiwa kupita njia hiyo ya umeme mkubwa wa kV 400 ili kujiridhisha na madai ya wananchi hao.

Na Nuru Mwasampeta, Dar es Salaam.