Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema hataki kusikia nishati ya umeme inakuwa kikwazo kwa vituo vya afya kushindwa kutoa huduma kwa wananchi.

Kauli hiyo ameitoa jana, Novemba 26 wakati wa ziara mkoani Iringa ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini na kuwasha umeme katika Wilaya kadhaa za Mkoa huo.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akikata utepe kuashiria uwashaji wa umeme katika kijiji cha Ikongosi wilayani Mufindi.

Alisema kipaumbele cha Serikali ni kuona maeneo ya kutolea huduma zikiwamo hospitali zinapatiwa umeme wakati wa utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme vijijini ili kunufaisha jamii na kuwa watakaoshindwa kutekeleza hilo hawatawavumiliwa.

“Wataalamu wanaosimamia miradi ya REA na TANESCO hii michepuko inawezekana, ukiangalia ramani na kuona maeneo ya kutolea huduma hayakuwepo kwenye orodha ya kupelekewa umeme mnaweza kuchepusha.”

“Kwa sasa tunajenga vituo vya afya zaidi ya 300 nchi nzima. Serikali tunataka vifanye kazi pale vinapokamilika, lakini hatutaki sekta ya nishati iwe kikwazo. Yaani Kituo cha afya kimejengewa Wodi ya upasuaji, kujifungulia, chumba cha kuhifadhi damu, halafu eti kituo kimekamilika lakini hakianzi kazi kwa sababu ya ukosefu wa nishati ya umeme. Naomba TANESCO mtambue upungufu huo hatutauvumilia.”

Alisema Wizara yake ilishaagiza kila Mkoa kupita kwenye vituo vya afya vinavyojengwa, kuboreshwa na kupanuliwa miundombinu kuangalia mahitaji na kujipanga kwa kuangalia namna ya kufikisha miundombinu ya umeme.

“Mhe Rais hatafurahi akisikia vituo vya afya vilivyojengwa viwe vimekamilika na vifaa vipo maana fedha zimeshalipwa MDS, eti hakijafunguliwa.”

Alisema pia Wizara yake ilishatoa maagizo kwa wasimamizi wa miradi ya REA na TANESCO kupeleka andiko la uchepushaji huo na kusisitiza kuwa hataki kusikia visingizio mikoani kwenye jambo hilo na tatizo hili lisijirejee.

Aidha, Mgalu alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria ifikapo mwaka 2020 inafikisha miundombinu ya nishati ya umeme katika kila eneo na ndiyo mana imekuwa ikiboresha baadhi ya vituo vya kuzalisha umeme na pia kuja na mradi mkubwa wa Kituo cha kuzalisha umeme megawati 2,100 Rufiji.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akikagua kituo binafsi cha kuzalisha umeme cha Mwenga ambacho kinazalisha megawati 4 na kuunganishwa katika vijiji 32 vya Wilaya ya Mufindi.

Alisema pia Serikali inatambua changamoto ya baadhi ya vijiji na vitongoji vimerukwa katika kuunganishwa na umeme na ndiyo maana imekuja na Mradi wa Ujazilizi kwenye mikoa 11 na ile yenye mahitaji makubwa ya umeme ikiwa ni baada ya kukamilika kwa majaribio yaliyofanyika mkoani Mara.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi alitaka Wizara kuangalia namna ya kufikisha umeme kwenye maeneo ya kutolea huduma kwa jamii kama hospitali, shule, mahakama na kueleza malalamiko ya wananchi kwa baadhi ya maeneo ambayo yamerukwa kufikishiwa umeme.

“Wananchi wamekuwa na shauku ya kutaka kufikishiwa umeme, lakini baadhi ya maeneo yamerukwa jambo ambalo limeibua manung’uniko hasa wakihofia kuwa watafikishiwa umeme wakati gharama zimeongezeka tofauti na sasa ambapo wanatakiwa kulipia Sh 27,000 tu,” alisema.

Akifafanua suala hilo, Mgalu alisema Mkoa wa Iringa  ni miongoni mwa mikoa ambayo itanufaika na miradi kadhaa ya umeme ambayo takribani vijiji 179 ikiwa ni pamoja na vijiji na vitongoji 410 vitanufaika na mradi wa ujazilizi.

Aidha, Mgalu pia alifikia ofisi za Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Iringa, na kuwataka viongozi wa CCM na wanachama mkoani humo kuwa mstari wa mbele kuunga mkono juhudi za Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan za kulinda na kuhifadhi mazingira.

“Kuna wanaosema kuwa mradi wa kuzalisha umeme wa Rufiji hautakuwa na maji, lakini hili si kweli na tunatakiwa kuanza sasa kulinda mazingira na maeneo oevu. Tukifanya hivyo mvua zitanyesha na maji yatapatikana na mradi wetu utafanikiwa.

Aidha, katika tukio la kuwasha umeme katika kijiji cha Ikongosi, Mufindi Kaskazini, Mahmoud Mgimwa ambaye taarifa yake ilisomwa kwenye mkutano huo alisema kilio cha wananchi wake ni kuongeza wigo wa kuunganisha umeme na kutaka kuongezwa nguzo ili kuwafikia wananchi wengi.

Naye mkazi wa kijiji hicho, Jeremia Sanga alishukuru Serikali kwa kuwafikishia umeme ambao alisema utakuwa chachu ya kuwabadilisha kimaisha.

 

 

coreldraw kaufen