Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuongeza nguvu ya umeme katika vijiji vyote nchini vyenye uhitaji mkubwa wa umeme.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) akiwasha huduma ya umeme katika kijiji cha Mwabakima katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV backbone (BTIP) katika Wilaya hiyo.

Mgalu alitoa agizo hilo wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa usambazaji umeme vijijini na kuwasha huduma ya umeme vijijini kupitia mradi wa njia ya kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV Backbone (BTIP) katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora pamoja na kukagua  utekelezaji wa mradi wa REA III awamu ya kwanza.

Mgalu alitoa agizo hilo baada ya kutembelea Kijiji cha Mwamashimba chenye mahitaji makubwa ya umeme baada ya  wanakijiji kuanzisha viwanda vidogodogo zikiwemo mashine za kusaga na kukoboa nafaka, mashine za kukamua mafuta yatokanayo  na mbegu   pamoja kuwepo kwa shughuli nyingi za uchomeleaji vyuma.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu(kulia) akisoma ujumbe uliowasilishwa kwake kwa njia ya mabango na wanakijiji wa kijiji cha Mwabakima katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa usambazaji wa umeme vijijini kupitia mradi wa kusafirisha umeme mkubwa wa 400kV backbone (BTIP) katika Wilaya hiyo.

“Hapa Mwamashimba  kunahitajika umeme zaidi, watu wamejiajiri kwelikweli, wanafanya shughuli za maendeleo, hii ndiyo sera ya Serikali ya awamu ya Tano, kwamba umeme uwafikie wananchi na uwanufaishe kwa kubadili maisha yao, transfoma mliyofunga haikidhi mahitaji kwani  shughuli zao ni nyingi mno,” alisema Mgalu.

Aliiagiza  TANESCO kuongeza  transfoma nyingine yenye uwezo mkubwa wa 200kV, kutoka 100kV ya sasa.

Katika ziara hiyo, Mgalu aliwataka wananchi waliopitiwa na mradi wa BTIP kujiandaa kwa kusuka nyaya katika nyumba zao ili mkandarasi anapopita katika maeneo yao wawe tayari kuunganishwa na huduma hiyo kwa bei nafuu ya 27,000.

Aidha aliwatoa hofu wananchi wote wa maeneo husika kuwa  watapata huduma ya umeme kwa kuwa  tayari wakandarasi wamefanya upimaji na kuwa na ramani ya utekelezaji, usambazaji na uunganishaji wa umeme katika Vijiji vyote vilivyopitiwa na BTIP.

Vilevile aliwaasa wananchi  kuendelea kutunza na kuilinda miundombinu ya umeme zikiwemo nguzo  kwa kutozichoma moto, kutoiba vifaa mbalimbali vya miundombinu hiyo pamoja na kulima kwa njia salama katika majaruba.

Sambamba na hilo aliwataka wananchi hao pamoja na wakandarasi kushirikiana pamoja katika kutekeleza  mradi huo katika maeneo yao, pia wananchi wa eneo husika wapatie fursa ya ajira kulingana na uwezo wao wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

Akiwa wilayani humo, Mgalu aliwasha huduma ya umeme katika vijiji vya Mwabakima na Mwashimba ambapo katika Kijiji cha Jogohya, Mgalu alikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na kumtaka mkandarasi kutoka kampuni ya OK, kuharakisha kazi ya kujenga miundombinu kwa kuwa wananchi wengine wamekuwa wakiusubiri mradi huo kwa shauku kubwa.

Na Zuena Msuya