Wataalam wa TANESCO punguzeni urasimu katika kutoa huduma ya nishati kwa wananchi, kazi zetu sisi ni sawa na kazi za polisi, kufanya kazi usiku na mchana.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameyasema hayo jana, Julai 20, wakati akiendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya REA III katika mikoa ya Geita na Mwanza katika Kata ya Madukamatatu wilayani Sengerema.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akihutubia wananchi wa Kata ya Madukamatatu Wilayani Sengerema.

“Sitarajii wataalamu wetu kuendelea kufanya kazi kwa mazoea, vinginevyo atapoteza kazi yake haraka sana.” Alisema Waziri Kalemani.

Akizungumza katika Mkutano huo, Waziri Kalemani amewaagiza Wakandarasi wote wanaotekeleza Miradi ya REA III Awamu ya Kwanza kukamlisha miradi hiyo ndani ya muda waliopangiwa kwa kuwa, hatutawaongezea muda.

Pia, Waziri Kalemani katika mkutano huo amewahimiza wananchi wote nchini kufanya wiring majumbani mwao na kuunganishiwa umeme.

“Lipeni kiasi cha shilingi 27,000 ili muunganishiwe umeme, kama hamna hiyo pesa, uzeni mbuzi au kondoo ili mpate pesa hiyo muwekewe umeme.” Alisema Waziri Kalemani.

Aidha, alielezea jinsi Wizara ya Nishati na Taasisi zake zinavyoendelea kuboresha huduma na kupeleka nishati ya umeme kwa wananchi, ingawa kuna changamoto ya kubadili miundombinu iliyochakaa.

Waziri Kalemani alisema kuwa, hadi sasa nimeambiwa kwamba vimebakia vijiji 68 ili wilaya yote ya Sengerema kupata umeme wa REA III. Na hivyo vijiji vilivyobakia vyote vitapelekewa umeme kupitia Mradi wa REA III Awamu ya kwanza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole amempongeza Waziri wa Nishati kwa kazi kubwa anayoifanya na kusema kuwa katika Wilaya ya Sengerema tayari vijiji 102 vimepata Umeme wa REA na vimebakia vijiji 68 ambavyo vitapata umeme kupitia REA III Awamu ya Kwanza.

Ameongeza kusema kuwa, wakati akianza kazi katika Wilaya ya Sengerema 2016 tatizo la kukatika katika kwa umeme lilikuwa ni kubwa lakini kwa sasa kuna mabadiliko makubwa sana.

Wananchi wa kijiji cha Kang’washi wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani.)

“Kwa mwezi mzima tunaweza tusipate changamoto ya kukatika katika kwa umeme kwa kweli tunakupogeza sana Waziri wa Nishati, Dkt. Kalemani.” Alisema Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Kipole.

Mkutano huu umehudhuriwa na Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati, REA, TANESCO, Uongozi wa Wilaya ya Sengerema pamoja na wanachi.

Na Rhoda James – Sengerema