Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga, wameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, changamoto walizonazo katika utekelezaji wa jukumu lao kuu la kusambaza huduma ya umeme kwa jamii.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa wamefuatana na waandishi wa habari, wakishuhudia nyumba ya mkazi wa kijiji cha Negezi wilayani Kishapu, ikiwashiwa umeme baada ya kuunganishiwa huduma hiyo, Machi 16 mwaka huu.

Akiwasilisha taarifa ya shirika hilo kwa Kamati husika, wakati wa ziara yao ya kazi mkoani humo Machi 16 mwaka huu, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Meneja wa TANESCO wa Mkoa, Mhandisi FedGrace Shuma alitaja changamoto mojawapo kuwa ni pamoja na uwepo wa vijiji kadhaa ambavyo havitafikiwa kikamilifu na huduma ya umeme kupitia mradi wa umeme vijijini awamu ya tatu (REA III) mzunguko wa kwanza.

“Tumepanga kuviingiza vijiji hivyo kwenye mradi wa REA awamu ya tatu – mzunguko wa pili,” alisema.

Aidha, alitaja changamoto nyingine kuwa ni uwepo wa maeneo mengi ndani ya Halmshauri za miji ya Kahama, Kishapu na Shinyanga ambayo hayajafikiwa na huduma ya umeme. Alisema kuwa, katika kukabiliana na hali hiyo, Wizara kupitia TANESCO kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wanaandaa mradi wa Peri-Urban Electrification, ili kuyafikia maeneo husika.

Changamoto nyingine iliyoelezwa ni kuwa, kwa mahitaji halisi ya umeme katika mji wa Kahama ikilinganishwa na ukuaji wa kasi wa mji huo, transfoma iliyopo imeanza kuzidiwa. “Kwa sasa matumizi ya juu ya kituo hicho ni megawati 22.6 za umeme wakati kituo kina uwezo wa kutoa megawati 24 tu,” alisema. Aliongeza kuwa, ili kukabiliana na changamoto husika, Wizara kupitia TANESCO ipo kwenye mipango ya kuongeza uwezo wa kituo.

Vilevile, Mhandisi Shuma alitaja changamoto nyingine kuwa ni malimbikizo ya Ankara za umeme mkoani humo, ambayo yamefikia jumla ya shilingi bilioni 1.63.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack (mwenye koti jeusi) na Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu (kulia), wakifurahia pamoja na wananchi wa Kijiji cha Bulimba, Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga baada ya kuwashwa umeme kwenye moja ya makazi ya wananchi, wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, Machi 16 mwaka huu.

Alifafanua kuwa, deni la taasisi za serikali ni shilingi bilioni 1.262 na deni la wateja binafsi shilingi milioni 370.4. “Wizara imetoa maelekezo kwa TANESCO kuhakikisha madeni yote yanakusanywa kwa wakati, ambapo shirika linaendelea na operesheni KATA UMEME kuhakikisha madeni yote yanalipwa na kwa wale watakaoshindwa kulipa madeni yao wafikishwe mahakamani.

Ikiwa mkoani Shinyanga, Kamati ilikagua miradi ya umeme katika vijiji vya Negezi, Bulimba na Mwaweja.