Serikali imelitaka Shirika la Umeme Tanzania  (TANESCO) kuweka bei elekezi kwa wakandarasi,wahandisi  na mafundi waliowaidhinisha kuwatandazia nyaya wananchi walio vijijini ili kuepusha matapeli na vishoka wanaowalaghai wananchi hao na kufanya kazi hiyo kwa gharama kubwa ukilinganisha ukubwa wa nyumba.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu akiwasha umeme katika moja ya Nyumba ya mwanakijiji wa kijiji cha Buha,wilayani Mbulu mkoani Manyara, alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini REA na kuwasha umeme katika baadhi ya kaya za vijiji vya wilaya hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA) pamoja kuwasha umeme katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara.

Mgalu alisema kuwa, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakitozwa gharama kubwa za kutandaza nyaya katika nyumba zao kutoka kwa mafundi wanaofanya kazi hiyo licha ya gharama za kuunganishwa na umeme kuwa bei nafuu ya 27,000.

Alisema baadhi ya mafundi wamekuwa wakiwalaghai wananchi  kuwa hata mita namba inatakiwa kulipiwa gharama wakati wa kuwekewa hali ya kuwa mita hizo zinatolewa bure kwa wateja wote wanaounganishwa na umeme wa REA.

Aliweka wazi kuwa,  ni marufuku kwa mkandarasi au Fundi anayeunganisha wateja kupitia mradi wa REA, kumtoza mwananchi gharama za gguzo, fomu, mita namba pamoja kifaa cha umeme tayari (UMETA) wakati wa utekelezaji wa mradi huo unaoendelea katika eneo husika.

“Hawa vishoka na matapeli wanasababisha wananchi wasiiamini Serikali yao sikivu ya kuwahudumia wanyonge, wengine wanaogopa kulipia gharama za kuunganishwa hasa wale wenye nyumba inayohitaji kutandazwa nyaya kutokana na gharama kubwa, kwa hali ya kawaida haiwezekani mtu anavyumba viwili au vitatu anatozwa laki nne mpaka milioni, TANESCO tuwasaidie wananchi wa vijijini wanufaike na umeme, na nyie wananchi wekeni mitego ya kuwamata vishoka washughulikiwe,” Alisisitiza Mgalu.

Alirejea kusema kuwa,  wasimamizi wa REA katika utekelezaji wa mradi huo, wasikubali visingizio vitakavyotolewa na mkandarasi yeyote kwa lengo la kuchelewesha mradi huo na kwamba hakuna muda utakaoongezwa kwa mkandarasi endapo atashindwa kukamilisha kwa wakati.

Naibu waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wanakijiji wa kijiji cha Buha,wilayani Mbulu mkoani Manyara, alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini REA na kuwasha umeme katika baadhi ya kaya za vijiji vya wilaya hiyo.

Vilevile aliwasisitiza wakandarasi hao kufanya kazi kwa majibu wa mkataba uliowekwa baina yao na Serikali katika kutekeleza mradi huo ili wakamilishe kwa wakati.

Mgalu alitoa wito kwa Wakazi wa  Wilaya ya Mbulu kuwa na mahusiano mazuri, ushirikiano kati yao na wakandarasi wanaotekeleza mradi wa kusambaza umeme vijijini REA katika Wilaya hiyo.

Katika Kijiji cha Buha wilayani Mbulu  wateja 3 Kati ya 25 wameunganishwa na umeme na Katika Kijiji cha Masqaroda  wateja 5 Kati ya 44 Wameunganishwa ambapo zoezi la kuwaunganisha wateja wengine litaendelea, huku wananchi wakisisitizwa kulipia huduma hiyo na kuweka tayari nyumba zao kupata huduma ya umeme.

Na Zuena Msuya