Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewapongeza wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kupeleka umeme kwa Kiwanda cha kuzalisha Nondo Kamal Industrial kilichopo Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili kulia) mara baada ya kuwasili katika Kiwanda cha Kamal kilichopo ndani ya eneo la EPZ Bagamoyo mkoani Pwani ili kukagua transforma pamoja na nguzo ambayo inapeleka umeme wa MW 22 katika kiwanda hicho.

Waziri wa Nishati ameyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda hicho mkoani Pwani jana tarehe 6 Agosti, 2018.

“Hongereni TANESCO kwa kuunganisha nishati ya umeme katika kiwanda hiki cha Kamal na hii kazi imefanyika ndani ya miezi miwili hongereni sana,” alisema Waziri Kalemani.

Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kuwa, Viwanda vyote na Taasisi za Umma zinaunganishwa na umeme wa kutosha na kwa wakati, alieleza Waziri Kalemani.

Aidha, Waziri Kalemani alisema kuwa, nimeelezwa kuwa kiwanda hiki kinaajiri takriban wafanyakazi 3000 na ni imani yetu kuwa kwa kuwa mmepata umeme wa kutosha na wa uhakika mtaajiri wafanyakazi wengi zaidi ya hao mlionao sasa, alisema Waziri Kalemani.

“Nyinyi mmeomba umeme wa MW 20 lakini sisi tumewaletea MW 22 na niimani yetu kuwa sasa umeme huu utakidhi mahitaji yenu,” alisema Waziri Kalemani.

Akizungumza katika ziara hiyo Waziri Kalemani alisema kuwa, “tumeamua kuwaunganisha na nishati hii ya umeme ili mvutie wawekezaji wengi zaidi katika eneo hili la EPZ ili viwanda vyote vitakavyoazishwa huku vikute tayari kuna nishati ya umeme ya kutosha”.

Muonekano wa nguzo za umeme ambazo zinapeleka umeme kutoka laini ya Tegeta kwenda kwenye kiwanda cha Kamal cha kuzalisha Nondo kilichpo Bagamoyo mkoani Pwani.

Waziri Kalemani alitoa wito kwa mmiliki wa Kampuni hiyo ya Kamal, Gagan Gupta kuhakikisha kuwa wanahamasisha wadau wengi zaidi ili waazishe viwanda katika eneo hilo la EPZ kwa kuwa sasa wanao umeme wa kutosha.

Kwa upande wake, mmliki wa Kiwanda cha Kamal, Gagan Gupta alisema kuwa, anapongeza na kumshukuru Waziri wa Nishati kwa jitihanda zake za kuhakikisha kuwa wanapata umeme wa kutosha kwa kuwa tumekuwa na tatizo la kukatika katika kwa umeme tatizo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu sasa.

“Ni furaha yangu kuwa sasa tatizo la miaka saba leo limifika tamati na umeme sasa ninao wa kutosha”, alisema mmliki Gagan Gupta.

Aidha ziara hii imeshirikisha Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati, TANESCO, REA na Viongozi kutoka kiwanda cha Kamal Industry.

Na Rhoda James – Pwani