Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupeleka umeme katika Wizara kumi ambazo bado hazijalipia gharama ya kuunganishiwa umeme katika maeneo yao ya ujenzi kwenye Mji wa Serikali uliopo Ihumwa jijini Dodoma.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (mwenye shati la bluu) akizungumza na wafanyakazi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wanaofanya kazi ya kusambaza umeme katika Mji wa Serikali, Ihumwa jijini Dodoma.

Ameyasema hayo leo jijini Dodoma baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme na ujenzi wa majengo ya Serikali katika eneo hilo la Ihumwa ambapo aliambatana Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua.

Baadhi ya viongozi wengine alioambatana nao ni Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga.

Dkt. Kalemani amesema kuwa, Serikali imetoa transfoma kwa ajili ya kufungwa katika maeneo ya wizara zote 22 kwenye Mji wa Serikali ili kazi za ujenzi zifanyike usiku na mchana na hivyo kuwezesha ujenzi wa majengo kukamilika mwisho wa mwezi huu kama ilivyopangwa.

“ Tumeshatoa transfoma, na tunatarajia zifanye kazi, hivyo nimewaelekeza wataalam wangu kuwa pamoja na kwamba hizo Wizara hazijalipia gharama, transfoma zifungwe katika maeneo yao ndani ya siku Tatu na Wizara hizo zianze  kutumia umeme huo ndani ya Siku Tano kwani malipo ni 921,000 tu,” amesema Dkt Kalemani.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (katikati), Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (wa kwanza kushoto) na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Nishati, Raphael Nombo (wa kwanza kulia), wakikagua kazi ya usambazaji umeme katika Mji wa Serikali, Ihumwa jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa,  jumla ya Wizara kumi ambazo tayari zimeshalipia umeme, Tanesco wanafanya kazi ya kuunganisha  nishati hiyo, ndani ya siku mbili.

Kuhusu maendeleo ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Nishati,  amemuagiza mkandarasi ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuongeza kasi ya ujenzi ili jengo hilo liwe limekamilika ifikapo tarehe 30 mwezi huu.

Aidha, ameeleza  kuwa, atakuwa akikagua kazi ya ujenzi wa jengo kila baada ya siku Tano ili kuona kama linaenda kwa kasi na ubora  kwa kuwa  mkandarasi huyo amekwilipwa fedha.

Na Teresia Mhagama

7/1/2019

windows 10 pro kaufen