Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani amesema kuwa Tanzania bado inavutia katika uwekezaji wa mafuta na gesi; hivyo amewakaribisha wawekezaji kuendelea kujitokeza kuja kuwekeza katika sekta husika.

Aliyasema hayo Septemba 25, 2018 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Kongamano la Pili la Mafuta na Gesi lililofanyika kwa siku mbili ambapo watu takribani 340 kutoka nchi zaidi ya 75 duniani walishiriki.

Akitoa salamu za shukrani kwa washiriki, Waziri Kalemani ambaye alizungumza kwa mtindo wa majumuisho, alisema kuwa miongoni mwa mambo makuu matano yaliyojitokeza katika kongamano hilo ni ukweli usiopingika kuwa, bado nchi mbalimbali zina matamanio na makusudio makubwa kuja kuwekeza Tanzania katika sekta husika.

Aidha, alitaja jambo jingine kubwa lililobainika katika kongamano hilo kuwa imeonekana kwamba mfumo wa será na sheria za Tanzania, bado unavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.

“Sera na Sheria zetu siyo hasi bali ni chanya kwa pande zote mbili kwa maana ya kuwezesha kunufaika kwa Serikali lakini pia kwa upande mwingine Kampuni za uwekezaji zisipate hasara.”

Vilevile, alisema kuwa kongamano limebainisha kuwa bado kuna kiasi kikubwa cha rasilimali za mafuta na gesi hapa nchini kwa maana ya uwepo wa maeneo mengi ya kufanyia utafiti wa rasilimali hizo.

Akifafanua zaidi, Waziri alisema kuwa hilo ni jambo jema na kwamba Serikali imetumia nafasi hiyo kuwaeleza wawekezaji fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini hususan maeneo muhimu kama Eyasi – Wembele kutoka Singida mpaka Tanga ambako ni muhimu sana kwa uwekezaji wa mafuta na gesi.

Alisema, eneo jingine ni Ziwa Tanganyika ambako dalili za mafuta na gesi bado zipo, lakini pia Ziwa Nyasa ambako kuna fursa za uwepo wa mafuta pamoja na sehemu nyingine kadhaa.

Waziri pia alitaja suala la umuhimu wa uwazi katika uwekezaji kuwa limejitokeza na kujadiliwa katika kongamano hilo. Alisema kuwa, Serikali, kwa kuona umuhimu wa suala hilo, ilipitisha Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji ya mwaka 2015.

“Sisi kama Serikali, bado tunazitaka Kampuni za uwekezaji ziwe wazi kuonesha manufaa wanayopata,” alisisitiza.

Alisema, suala la ushirikishwaji wa Watanzania katika miradi mbalimbali ya uwekezaji wa mafuta na gesi ni muhimu sana na kwamba pia lilizungumzwa katika kongamano.

Meza Kuu, wakiongozwa na Waziri wa Nishati Dkt Mrdard Kalemani (katikati), wakishiriki katika Kongamano la Pili la Mafuta na Gesi lililofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 24 na 25, 2018.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kufunga kongamano  na kufafanua zaidi kuhusu nafasi ya watanzania kuwekeza katika sekta hiyo muhimu, Waziri alibainisha kuwa, ni lazima watanzania watambue kuwa uwekezaji katika sekta hizo unahitaji teknolojia kubwa na uwezo mkubwa wa mtaji. “Kupata mafuta siyo jambo dogo. Unaweza ukatafuta mafuta kwa miaka 20 na usipate.”

Hata hivyo, Waziri alisema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada za makusudi katika kuwawezesha Watanzania kunufaika na sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kuweka mfumo wa será inayowapa kipaumbele wazawa kushiriki katika uwekezaji.

Pia, alisema Serikali imeweka mfumo wa kisheria unaoweka mazingira rafiki kwa watanzania kuweza kushiriki katika uwekezaji.

“Mathalani, kwenye Sheria ya Mafuta ya mwaka 2015, tumeweka kipengele mahsusi kinachomtaka mwekezaji wa nje amshirikishe Mtanzania kwa hisa zisizopungua asilimia 25,” alifafanua Waziri.

Akitoa tathmini ya kongamano hilo, Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt Hamisi Mwinyimvua, alisema kuwa limekuwa lenye ufanisi wa hali ya juu, ambapo Serikali imepata fursa ya kunadi fursa za uwekezaji kwa wadau walioshiriki kutoka nchi mbalimbali duniani.

Kutoka kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt Hamisi Mwinyimvua, Afisa Mwandamizi kutoka wizarani Adam Zuberi na Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Petroli Mhandisi Joyce Kisamo, wakiwa katika siku ya pili ya Kongamano la Mafuta na Gesi lililofanyika jijini Dar es Salaam, Septemba 24 na 25, 2018.

“Tumeeleza utayari wetu wa kushirikiana na sekta binafsi katika uwekezaji kwenye sekta hizi muhimu za mafuta na gesi. Pia, tumeweza kubadilishana mawazo na uzoefu. Ni matarajio yetu kupokea maombi mengi zaidi ya uwekezaji, hali ambayo italinufaisha Taifa.”

Naye mwandaaji mkuu wa kongamano hilo, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Wawekezaji wa Mafuta na Gesi Tanzania (ATOGS), Abdulsamad Abdulrahim, aliipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati, kwa ushirikiano ambao imeendelea kuuonesha kati yake na sekta binafsi katika kukuza sekta husika kwa manufaa ya watanzania.

Kongamano hilo la pili, lilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali, akiwemo Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu; Waziri wa Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati-Zanzibar, Salama Talib; Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Binilith Mahenge na wengine wengi kutoka Wizara, Taasisi za Serikali na Taasisi Binafsi.

Na Veronica Simba