Mtaalam Mwelekezi aliyeingia Mkataba na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kufanya Tathmini ya Mazingira (EIA) katika Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji ya Mto Rufiji Profesa Raphael Mwalyosi, amesema kuwa athari za kimazingira zilizobainika kuweza kutokea, zinaweza kuzuilika.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua (kulia) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Prof Simon Msanjila, wakifuatilia uwasilishwaji wa Tathmini ya Mazingira ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji ya Mto Rufiji, Juni 11, 2018 Dodoma.

Ameyasema hayo leo, Juni 11, 2018 wakati akiwasilisha Tathmini hiyo ya Mazingira kwa Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali zenye majukumu ya kutekeleza miundombinu wezeshi ya Mradi husika.

“Tathmini yetu imebainisha kuwa Mradi husika unaweza kutekelezwa pasipo shaka yoyote kwani athari zake kimazingira zinaweza kuzuilika. Muhimu ni kuweka mikakati ya kuzizuia,” alifafanua.

Uwasilishwaji wa Tathmini ya Mazingira kwa Kamati hiyo Tendaji, umefanyika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati jijini Dodoma, ambapo ni moja ya hatua muhimu zinazoendelea kufanyika kabla ya kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi huo.

Wajumbe walioshiriki katika zoezi la uwasilishwaji wa Tathmini husika ni Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi;  Maliasili na Utalii; Mambo ya Ndani ya Nchi, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki; Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo; Kilimo; Mifugo na Uvuvi pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Nyingine ni Wizara ya Fedha na Mipango; Ofisi ya Makamu wa Rais – Mazingira; Ofisi ya Waziri Mkuu; Wizara ya Madini pamoja na Wizara ya Nishati, ambayo ndiyo yenye dhamana.

Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali zenye majukumu ya kutekeleza miundombinu wezeshi ya Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu ya maji ya Mto Rufiji, wakimsikiliza Mtaalam Mwelekezi, Prof Raphael Mwalyosi (aliyesimama), alipokuwa akiwasilisha Tathmini ya Mazingira ya Mradi husika, Juni 11, 2018 Dodoma.

Aidha, wadau wengine walioshiriki ni Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Wakuu wa Taasisi za Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania (TAWA), Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na TANESCO.

Na Veronica Simba – Dodoma