Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Beatus Segeja ametembelea eneo la Ibadakuli lililoko Manispaa ya Shinyanga ilikufahamu matokeo ya Tafiti za awali za Nishati ya Jotoardhi na mpango wa TGDC wa kufanya tafiti za kina katika eneo hilo.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi, Kato Kabaka (kulia) akitoa maelezo ya utafiti wa awali wa nishati ya jotoardhi mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya TGDC Beatus Segeja, katika eneo lenye viashiria vya nishati ya jotoardhi, Kata ya Ibadakuli nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga.

Akipata maelezo kutoka kwa Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Kato Kabaka, amesema tafiti za awali zinaonesha uwepo wa nishati ya jotoardhi inayoweza kutumika kwa matumizi mbali mbali tafiti za kina zikikamilika.

“Tayari tafiti za awali za eneo hili zinaonesha linafaa zaidi kwa matumizi ya moja kwa moja kama utalii, kilimo na ufugaji,” alifafanua Mhandisi, Kabaka.

Ameongeza kuwa, kiwango cha joto kilichopo katika eneo husika kwa sasa kiko chini kuweza kuzalisha umeme, ingawa tafiti za kina zikifanyika zitatoa jawabu sahihi kama nishati hiyo inaweza kufaa kuzalisha umeme.

“Kwa sasa tutaongeza msukumo wa tafiti katika eneo hili ili kupata taarifa nyingi za kisayansi zitakazo tusaidia katika kufanya maamuzi ya miradi sahihi ambayo kiuchumi inafaa kuwekeza katika eneo hili,” alieleza Mhandisi, Kabaka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TGDC, Beatus Segeja alisema kuwa ipo haja ya TGDC kuongeza nguvu zaidi katika kuhakikisha taarifa za kina za utafiti zanapatikana ili kuwa na uhakika wa aina ya miradi inayofaa kuwekeza katika eneo hilo.

“Iwapo tafiti zikikamilika na kuonyesha uwepo wa jotoardhi mahali hapa, eneo hili ni rahisi kufikika na lina tija kibiashara kwani liko karibu na Manispaa ya Shinyanga, zaidi liko karibu na barabara ya Shinyanga kwenda Mwanza,” alisisitiza, Segeja.

Mchumi, kutoka TGDC, Erasmus Hyera (kulia) akielezea manufaa ya kiuchumi yanayoweza kupatikana katika mradi wa jotoardhi mbele ya Mwenyekiti wa Bodi ya TGDC, Beatus Segeja, eneo la Ibadakuli nje kidogo ya Manispaa ya Shinyanga

Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi nchini (Tanzania Geothermal Development Company Limited) TGDC ni Kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) iliyoanzishwa kwa lengo kuu la kusimamia, kutafiti, kuvuna na kuendeleza jotoardhi (Geothermal energy) nchini ili kuongeza vyanzo vya nishati ya umeme pamoja na matumizi mengine ya moja kwa moja.

Augustino Kasale – TGDC