Serikali imesema kuwa taratibu za ufungaji wa mita za kupimia mafuta ( flow meter) katika bandari zote nchini ziko katika hatua za mwisho baada ya taratibu zote za awali kukamilika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja ( PBPA), Mhandisi Erasto Simon (aliyesimama) akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu hali ya miundombinu ya kupokelea mafuta katika Bandari Kuu, Maghala ya kuhifadhi mafuta,  pamoja na mita za kupimia mafuta.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, jijini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyokuwa ikijadili taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu hali ya miundombinu ya kupokelea mafuta katika Bandari Kuu, Maghala ya kuhifadhi mafuta,  pamoja na mita za kupimia mafuta.

Kikao hicho kiliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula, ambaye alihoji masuala kadhaa kubwa likiwa ni hatua zilizofikiwa katika zoezi  za ufungaji mita hizo katika bandari kuu nchini ili kudhibiti upotevu wa mafuta na kuongeza mapato ya Serikali.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani alieleza kuwa tayari hatua mbalimbali zimekwishachukuliwa ili kukamilisha zoezi hilo, baada ya Mawaziri wa wizara tano, zinazoshirikiana katika sekta hiyo kukutana pamoja na kuweka ratatibu za kuimarisha na kudhibiti upotevu wa mafuta.

Dkt. Kalemani alieleza kuwa, kwa sasa mita zipo kwenye mchakato wa manunuzi, ambapo zoezi hilo linakwenda haraka na muda si mrefu litakamika na kulitolea taarifa.

Baadhi ya watendaji wa Wizara ya Nishati na taasisi zilizochini yake wakiwa katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, kilichofanyika jijini Dodoma.

“ Zoezi la kununua Flow Meter linaendelea vizuri na kwa kasi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ndiyo ilipewa jukumu la kusimamia zoezi hilo, kwa kuwa sekta hii inahusisha Wizara tano, ikiwemo Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda na Wizara ya Nishati yenyewe:, ufungaji wa flow meter hizo utafanyika katika bandari zote nchini ikiwemo Dar es salaam, Tanga pamoja na Mtwara”, alisisitiza Dkt. Kalemani.

Kuhusu suala la upokeaji wa mafuta kwa pamoja, Dkt. Kalemani alisema, kupitia Wakala wa Serikali wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja ( PBPA)  na kampuni zinazofanya biashara ya mafuta nchini ( OMCs) unaendelea kukamilisha  taratibu za kuanzisha  mfumo wa upokeaji wa mafuta sehemu moja unaofahamika kama Single Receiving Terminal (SRT).

Alisema kuwepo kwa utaratibu huo kutapunguza muda wa meli kusubiri kushusha mafuta hivyo kupunguza upotevu wa mafuta.

Pia PBPA kwa kushirikiana  na Taasisi za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji( EWURA) pamoja na OMCs unaendelea kuimarisha mfumo wa kitaalam ili mabomba yote yaunganishwe kwenye mfumo ulio rahisi kuuendesha kwa lengo la kuboresha sekta hiyo.

Akizungumzia wa kampuni ya kuhifadhi mafuta ya TIPPA, pamoja na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania( TPDC) Dkt. Kalemani alisema kuwa kinachofanyika sasa ni kuangalia uwezekano wa kupanua miundombinu ili ilingane na uhitaji wa mafuta .

Aidha aliwaeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa, wameweka mfumo wa  kieletroniki ili kulinda mindombinu ya  mabomba yanayotoka baharini kuelekea kwenye maghala ya kupokelea mafuta ili yasitobolewe.

Mfumo huo wa kieletroniki utakuwa ukitoa taarifa iwapo msukumo wa mafuta utapungua wakati wowote wa zoezi la upakuaji wa mafuta.

Na Zuena Msuya

25/10/2018