Ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), umetembelea Kituo cha kupooza umeme kilichopo Zuzu mkoani Dodoma ambacho ni miongoni mwa vilivyo katika mpango wa upanuzi wake kwa ufadhili wa Benki hiyo na wadau wengine wa maendeleo.

Ziara hiyo ilifanyika Aprili 11, mwaka huu baada ya kufanya mazungumzo na Serikali kujadili maendeleo ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki hiyo; ambapo kwa upande wa nishati, Waziri mwenye dhamana, Dkt. Medard Kalemani alishiriki pamoja na wataalam wa wizara na TANESCO.

Akifafanua kuhusu ufadhili huo; Afisa Nishati Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Salum Inegeja alisema kwa upana wake, unahusisha Mradi wa ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 400 umbali wa kilomita 670 kutoka Iringa hadi Shinyanga pamoja na upanuzi wa vituo vinne vya kupoza umeme kwenye miji ya Iringa, Dodoma, Singida na Shinyanga.

Aidha, alisema kuwa mradi huo uligharimu Dola za Marekani milioni 496 sawa na shilingi bilioni 991 za Tanzania; ambazo kati yake, AfDB imechangia Dola milioni 64.85 sawa na shilingi bilioni 130.

Na Veronica Simba – Dodoma.