Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kuwa mara baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa umeme utakaopelekea mikoa ya Njombe na Ruvuma kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa Septemba, 20 mwaka huu, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) litaweza kuokoa shilingi bilioni 30 zilizokuwa zikitumika kama gharama ya kuendesha mitambo ya kuzalishia umeme inayotumia mafuta mazito katika mikoa hiyo.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akielezea matumizi ya kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wananchi wa kijiji cha Suluti kilichopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma (hawapo pichani)

Waziri Kalemani aliyasema hayo mapema jana tarehe 04 Juni, 2018 kwa nyakati tofauti kupitia mikutano na vijiji vya Suluti kilichopo wilayani Namtumbo na Lukumbule na Mkowela vilivyopo wilayani Tunduru mkoani Ruvuma kwenye ziara yake ya kukagua njia ya Makambako – Songea, vijiji vinavyotakiwa kuunganishwa na umeme wa Gridi ya Taifa pamoja na miradi ya usambazaji wa umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)

Katika ziara hiyo Waziri Kalemani aliambatana na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Wakala wa Nishati Vijijini (REA), wakandarasi pamoja na wakuu wa wilaya husika.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, shirika la Tanesco limekuwa likitumia gharama kubwa ya shilingi bilioni 30 kwa mwaka kama  gharama ya uendeshaji wa mitambo inayotumia mafuta mazito katika mikoa ya Njombe na Ruvuma na kusababisha hasara badala ya faida.

Alisema kuwa, mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea mapema mwezi Septemba mikoa ya Njombe na Ruvuma itaunganishwa rasmi na Gridi ya Taifa na kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 30 kinachotumika kuendesha mitambo ya mafuta mazito gharama ambazo ni kubwa tofauti na mapato ya shirika hilo ya shilingi bilioni tisa kwa mwaka kwa mikoa husika.

Aidha, aliongeza kuwa kuingizwa katika Gridi ya Taifa kwa mikoa ya Njombe na Ruvuma kutapelekea uwepo wa nishati ya uhakika na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani aliwataka wananchi wa Ruvuma kujiandaa na fursa mbalimbali zitakazojitokeza mara baada ya uwepo ya nishati ya uhakika ya umeme kama vile viwanda.

Alisema kuwa, uwepo wa viwanda vya nafaka hasa maeneo ya vijijini kutapunguza wimbi la vijana kukimbilia mijini kwa ajili ya kutafuta ajira.

Akielezea miradi ya usambazaji wa miundombinu ya umeme inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Waziri Kalemani alisema kuwa serikali imeweka lengo la kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2021, kazi ambayo inafanywa kwa awamu tofauti.

Aliwataka wananchi kujiandaa na kuunganishiwa na huduma ya umeme kwa kutandaza mfumo wa nyaya majumbani (wiring) au kuweka kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa wenye nyumba ndogo ili waweze kuwekewa umeme kwa walati.

Alizitaka taasisi mbalimbali kama vile hospitali, shule, makanisa na misikiti kutenga fedha kwa ajili ya kutandaza mifumo ya umeme ili waweze kuwekewa umeme pindi kazi  inapoanza.

Aidha aliwataka wananchi kuepuka matapeli wanaowatoza fedha nyingi kwa ajili ya kuwekewa umeme na kusisitiza kuwa gharama ya kuunganishiwa huduma ya umeme ni shilingi 27,000 tu.

Sehemu ya wananchi wa kijiji cha Suluti kilichopo wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) alipokuwa akiwaelezea mikakati ya serikali katika upelekaji wa huduma ya umeme vijijini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Omela alitoa pongezi kwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kasi yake ya ufikishaji wa huduma ya umeme hasa maeneo ya vijijini.

Alisema mara baada ya mkoa wa Ruvuma kuingizwa kwenye  Gridi ya Taifa, uchumi wa mkoa utakua mara dufu kutokana na ongezeko la shughuli za madini na viwanda vya kubangua korosho.

Hata hivyo Omela alimwomba Waziri Kalemani kutoa kipaumbele katika upelekaji wa umeme katika kijiji cha Lukumbule kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji kutokana na ongezeko kubwa la watu na usalama.

“ Katika eneo la Lukumbule lililopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji mbali na uwepo wa watu wengi, kuna kituo cha uhamiaji ambacho kinahitaji umeme wa uhakika unaotokana na Gridi ya Taifa ili kuweza kufanya shughuli zake za kiusalama kwa ufanisi zaidi,” alisema Omela.

Na Greyson Mwase, Ruvuma