Katika kuhakikisha kuwa Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia inakuwa na wataalam wa kutosha watakaosimamia rasilimali hiyo katika hatua mbalimbali kama utafutaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji, Wizara ya Nishati imekuwa ikitafuta fursa mbalimbali za masomo kutoka nchi kama vile Brazili, Ufaransa na China ili watanzania wapate nafasi ya kupata ujuzi kutoka nchi hizo.

Katika mwaka wa Fedha 2012/2013, Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini inaingia Makubaliano na Serikali ya Watu wa China ili kutoa udhamini wa masomo ya fani ya Mafuta na Gesi kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu kwa Watanzania kila mwaka kwa kipindi kinachoishia mwaka 2019/2020.

Katika Makubaliano hayo, Serikali ya China inaahidi kutoa nafasi kumi (10) kila mwaka, lakini kwa kutambua umuhimu wa wataalam katika kusimamia rasilimali hii adimu, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015/2016 nafasi hizo zinaongezwa hadi kufikia ishirini (20).

Hii ni kusema kwamba, tangu mwaka 2013/2014 Serikali ya China ilipoanza kutoa ufadhili, Watanzania 100 wamepatiwa fursa ya masomo katika fani ya Mafuta na Gesi kwa Shahada ya Uzamivu na Uzamili.

Katika mwaka huu, tarehe 20 Agosti, 2018, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua, anashuhudiwa akikabidhi barua za udahili na kuaga vijana wa kitanzania 20 wanaoenda nchini China kusomea masuala ya mafuta na Gesi katika ngazi ya Shahada ya Kwanza, Uzamili na uzamivu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt Hamisi Mwinyimvua (katikati waliokaa), Mwakilishi wa Ubalozi wa China, Xu Chen (kulia kwa Katibu Mkuu) na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Nishati, Raphael Nombo wakiwa katika picha ya pamoja na vijana wa kitanzania waliopata ufadhili wa masomo kwenda nchini China kusomea Mafuta na Gesi.

Vijana wawili watasomea shahada ya kwanza, Watatu watasomea shahada ya uzamivu na 15 watasomea shahada ya uzamili. Hii ni kusema kwamba, Serikali ya China pia imeona umuhimu wa kusomesha vijana katika shahada ya kwanza badala ya uzamili na uzamivu tu.

Dkt. Mwinyimvua anaeleza kuwa, lengo la kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanashiriki katika kusimamia Sekta ya Mafuta na Gesi haliishii kwa kupeleka wanafunzi nchini China pekee bali hata vyuo vya ndani ya nchi vinatoa elimu hiyo na watanzania wengine wanapelekwa nchini Uingereza kusomea Sekta husika.

Mwakilishi wa Ubalozi wa China, Xu Chen pamoja na kutoa pongezi kwa vijana hao waliopata ufadhili, anasema kuwa sekta ya Mafuta na Gesi ni muhimu katika nchi zinazoingia katika uchumi wa viwanda kwani ni injini ya kuendesha viwanda hivyo.

Anasema kuwa, Tanzania imebarikiwa na rasilimali mbalimbali ikiwemo Mafuta na Gesi asilia hivyo inahitajika Watu wa kufanya shughuli mbalimbali ikiwemo utafutaji, usafirishaji na uchakataji.

Anaongeza kuwa, watanzania hao waliopata ufadhili ni miongoni mwa watakaofanikisha suala hilo.

Aidha, anawataka vijana hao kusoma kwa bidii na kuurudisha ujuzi nchini Tanzania ili nchi ione fahari na faida ya kusomesha Vijana hao pamoja kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Watu wa China na Tanzania.

Mchakato wa kuwapata Watanzania wanaopata ufadhili, huhusisha utoaji wa matangazo katika vyombo mbalimbali vya habari ili watanzania waombe ufadhili huo na baada ya kupokea maombi, Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Ubalozi wa China hushirikiana katika mchakato mzima wa uchambuzi wa majina yaliyokidhi vigezo vya kupata ufadhili husika.

Na Teresia Mhagama, MoE