Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ametuma ujumbe kwa watanzania kwamba utekelezaji wa mradi mkubwa wa kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda kupitia Tanga Tanzania hadi nchi za nje yatakakouzwa, haujasimama kama baadhi wanavyodhani.

Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Nishati (Tanzania), Dkt Medard Kalemani (wa nne kutoka kulia) na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini (Uganda) Mhandisi Irene Muloni (wa tatu kutoka kulia), wakiongoza mkutano wa tatu wa mawaziri wa sekta zinazosimamia mradi wa bomba la mafuta kutoka nchi za Tanzania na Uganda, uliofanyika Desemba 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wa tatu wa mawaziri wa sekta zinazosimamia mradi husika kutoka nchi za Tanzania na Uganda, uliofanyika Desemba 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam, Waziri Kalemani aliwataka kufikisha ujumbe huo kwa wananchi ili wajue hali halisi ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa.

“Nendeni mkawaeleze watanzania kwamba mradi huu haujasimama. Kimsingi ndiyo tumeongeza kasi katika kuutekeleza ili ukamilike kwa wakati kama tulivyojipangia,” alisema.

Akifafanua hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo, Waziri Kalemani alisema kwa upande wa Tanzania tayari wamekamilisha utafiti wa kijiolojia na kijiofizikia na sasa wanaendelea na uchimbaji wa mashimo ambamo bomba hilo la mafuta litalazwa.

Aidha, alisema kwamba kazi husika imeshafanyika katika mikoa ya Tanga na Manyara na sasa inaendelea katika Mkoa wa Dodoma, wilayani Kondoa.

Vilevile, alieleza kwamba tathmini zote za mazingira zimekamilika, taratibu za masuala ya fidia na ustawi wa jamii ambapo mradi utapita zimekamilika na hatua inayofuata sasa baada ya majadiliano kukamilika ni ujenzi.

Akijibu swali la mmoja wa waandishi kuhusu kuchelewa kwa mradi, Waziri Kalemani alifafanua kuwa, mradi haujachelewa kwani umeshaanza kutekelezwa. Alisema mradi unatekelezwa hatua kwa hatua.

“Tulisaini mkataba mwaka jana, tukaanza kupata maeneo, tukaanza kufidia upande wa Tanga, tumekamilisha utafiti wa mazingira, tumejua ukubwa wa bomba, tumeshaanza kuchimba mashimo ambapo bomba litalazwa. Yote hayo ni utekelezaji, kwahiyo hatujachelewa.”

Kuhusu kukamilisha majadiliano, Waziri Kalemani alisema kuwa wamejiwekea hadi Januari 17 mwakani wawe wamekamilisha.

Akifafanua zaidi, alisema kwamba majadiano yanatakiwa yawe ya manufaa kwa nchi, ndiyo maana hayawezi kukamilika kwa siku moja. Alisema, ili kuzingatia maslahi ya nchi, zipo hatua zinazohusisha kuwashirikisha wadau mbalimbali akitolea mfano kwa upande wa Tanzania, ni pamoja na kuainisha kampuni mbalimbali za ndani ili kuzijengea uwezo na kubainisha utaratibu wa namna ya kuzishirikisha ziweze kunufaika na mradi husika.

Makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali zinazohusika na mradi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Tanzania na Uganda, wakishiriki katika mkutano wa tatu wa Mawaziri wa sekta zinazosimamia mradi wa bomba la mafuta kutoka nchi za Tanzania na Uganda, uliofanyika Desemba 7 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Aidha, alisema ziko jamii za watanzania ambazo zinalengwa zinufaike na mradi husika na kwamba yako mapato yatokanayo na mradi ambayo yanapaswa yaingie kwenye Pato la Taifa, hivyo ni lazima majadiliano yazingatie taratibu zote ili mradi uwe wa manufaa.

Waziri Kalemani alisema kwamba, katika majadiliano yao na ujumbe kutoka Uganda ulioongozwa na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Mhandisi Irene Muloni, walikubaliana kuwa kila nchi ihakikishe inasimamia kwa nguvu zote uharakishwaji wa taratibu za msingi ili mradi uweze kutekelezwa haraka iwezekanavyo.

“Kwahiyo tumekubaliana kwamba wakati wowote mwakani, taratibu zote za maandalizi ziwe zimekamilika ili utekelezaji wa mradi katika hatua ya ujenzi uendelee.”

Kwa upande wake, Waziri Muloni alikubaliana na yote yaliyoelezwa na Waziri Kalemani na aliongeza kuwa, wamekubaliana kuharakisha mchakato wa hatua za maandalizi ili ujenzi ufanyike kwa wakati na kuwanufaisha wananchi wa nchi zote mbili kama ilivyokusudiwa.

Mkutano huo wa ngazi ya mawaziri, ulihudhuriwa pia na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu. Vivyo hivyo kwa upande wa Uganda, mawaziri kadhaa kutoka sekta zinazohusika na mradi huo walishiriki.

Aidha, mkutano huo ulitanguliwa na mkutano wa ngazi ya makatibu wakuu ulioongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua Desemba 6 na ngazi ya wataalamu uliofanyika Desemba 5 jijini Dar es Salaam.

Mkutano mwingine wa majadiliano umepangwa kufanyika Uganda, Januari mwakani.

Na Veronica Simba – Dar es Salaam.

avast kaufen