Uzinduzi wa utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme vijijini (REA III ) umekamilika katika mikoa yote nchini baada ya Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, kuzindua utekelezaji wa mradi huo katika Mkoa wa Katavi uliokuwa umesalia kati ya mikoa 26 nchini.

Akizungumza katika mikutano tofauti ya wanavijiji wa mkoa huo, ikiwemo vya Wilaya ya Tanganyika katika kijiji cha Chakasekese ambapo uzinduzi huo ulifanyika, Septemba 10, 2018, Dkt. Kalemani alisema kukamilika kwa uzinduzi katika Mkoa huo kutawezesha vijiji vyote vya Tanzania kuunganishwa na huduma ya umeme ifikapo 2021.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amos Makalla, (kushoto) akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme wa Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa huo. Kushoto kwake ni Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani.

Alisema katika Mkoa wa Katavi zaidi ya wateja 10,000 wataunganishwa na huduma ya umeme katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa REA III na kwamba zaidi ya vijiji 100 vitaunganishwa na huduma hiyo.

Aidha awamu ya pili inayoanza mwezi JulaI 2019 itahitimisha vijiji vyote vilivyosalia hadi kufikia 2021 na kufanya vijiji vyote kupata umeme Tanzania nzima.

Alifafanua kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji itachukua muda wa miezi 24.

Akiwa katika Wilaya ya Mlele katika Mkoa huo wa Katavi, katika Kata ya Majimoto, aliwataka wananchi wote wa mkoa huo kujiandaa kwa kutandaza nyaya katika nyumba zao ili mradi huo utakapofika katika maeneo yao waweze kuunganishwa kwa haraka .

Vilevile aliwasisitiza kuwa wasikubali kurubuniwa na wakandarasi au vishoka katika kutandaziwa  nyaya katika nyumba zao, bali watumie mafundi walioidhinishwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao majina yao yamebandikwa nje ya Ofisi za TANESCO.

Dkt.Kalemani aliwaeleza kuwa gharama za kuunganishwa na huduma ya umeme ni Shilingi 27,000 tu na endapo ikatokea mtu au kikundi anawaeleza bei tofauti na hiyo  watoe taarifa katika Ofisi za Serikali ya kijiji, TANESCO na Kituo cha Polisi ili mtu huyo achukuliwe hatua kwa kuwa ni kinyume na utaratibu uliowekwa.

Wakazi wa kijiji cha Maji Moto wilayani Mlele wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani hayupo pichani wakati akizungumza nao kuhusu kupeleka huduma ya umeme katika Mkoa wa Katavi.

Sambamba na hilo, aliwashauri kutumia kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kwa nyumba ambazo hazihitaji kutandazwa nyaya ili kupunguza gharama ya kuunganishwa na huduma ya umeme, ambapo aliwaeleza kuwa wateja 250 wa awali watapata vifaa hivyo bure, na baadaye kifaa hicho kitauzwa kwa bei ya Serikali ya Shilingi 36,000.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Katavi, Amos Makalla aliwataka  wananchi hao kuwa tayari kupokea mradi huo kwa kutoa maeneo yao na kuruhusu miti ikatwe ili kupitisha miundombinu ya mradi huo kwa kuwa hauna fidia kwa wananchi.

Makala alisema kuwa, wananchi wote washirikiane na wakandarasi kuharakisha utekelezaji wa mradi huo, kwa kutoa nguvu kazi pale itakapohitajika ukizingitia kuwa mkoa huo ndiyo wa mwisho katika Kuzindua utekelezaji wa mradi huo.

Wananchi wa mkoa huo wametakiwa kuchangamkia fursa ya ajira itakayopatikana wakati wa utekelezaji wa mradi na kwamba wawe waaminifu na kulinda vifaa pamoja na mali za mkandarasi zisiharibiwe wala kuibiwa na watu wasio waaminifu.

Hata hivyo mkandarasi anayetekeleza mradi katika mkoa huo ametakiwa kutochukua vijana wa kazi au vibarua nje ya mkoa husika ili kuwanufaisha kiuchumi wakazi wa eneo husika.

Na Zuena Msuya