Vijiji vya Iyula B, Mapogoro na Saza vilivyopo mkoani Songwe vimeanza kupata huduma ya umeme baada ya kuzinduliwa na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani tarehe 18 na 19, Mei, 2018.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akizungumza na Wananchi katika Kijiji cha Iyula B, wilayani Mbozi kabla ya kuzindua huduma ya upatikanaji wa umeme katika Kijiji hicho.

Dkt. Kalemani alizindua huduma hiyo baada ya kufanya ziara katika wilaya ya Songwe, Mbozi  na Ileje mkoani Songwe ambapo pia alizungumza na wananchi katika Vijiji mbalimbali katika Wilaya hizo.

Waziri wa Nishati, alisema kuwa, Wilaya ya Songwe ina Vijiji 43 ambapo ni vijiji 29 tu ambavyo havijasambaziwa umeme, hivyo vitasambaziwa umeme katika mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu (REA III) utakaokamilika mwezi Juni, 2021.

Aidha, akiwa katika Kijiji cha Udinde wilayani humo, alimuagiza mkandarasi wa umeme vijijini, kampuni ya Steg International kuhakikisha kuwa wanawasha umeme katika Kijiji hichop ifikapo Juni, 30 mwaka huu.

Akiwa wilayani Ileje na Mbozi, pia alitoa ahadi ya kusambaza umeme katika Vijiji vilivyosalia kupitia REA III, mzunguko wa kwanza unaokamilika Juni 2019 na Mzunguko mwingine utakaoanza Julai, 2019.

Dkt. Kalemani aliwataka Wananchi katika maeneo yote nchini kuhakikisha kuwa wanalinda miundombinu ya umeme ili kutorudisha nyuma juhudi za Serikali katika kusambaza nishati hiyo.

Viongozi mbalimbali walioambatana na Waziri katika ziara hiyo akiwemo Mbunge wa Ileje, Janet Mbene na Mbunge wa Songwe, Philipo Mulugo waliipongeza Serikali kwa juhudi inazofanya katika kusambaza umeme vijijini na pia walimpongeza Waziri wa  Nishati kwa juhudi zake katika kusimamia kwa karibu kazi ya usambazaji umeme vijijini.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kulia) akiwatambulisha kwa Wananchi wa Kijiji cha Iyula B, wilayani Mbozi, watendaji wa Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Mkandarasi anayesambaza umeme vijijini mkoani Songwe (Steg International) kabla ya kuzindua huduma ya upatikanaji wa umeme katika Kijiji hicho.

Na Teresia Mhagama, Songwe.