Mameneja wote wanaosimamia vituo vya kupoza na kusambaza umeme nchini wametakiwa kufanya ukaguzi ( checkup) wa kila siku asubuhi katika mitambo iliyopo kwenye vituo hivyo ili kuondoa adha ya kukatika umeme kunakotokana na hitilafu katika mitambo hiyo.

Ukaguzi huo unaenda sambamba na vituo hivyo kufanyiwa ukarabati  na ukaguzi wa mara kwa mara au hata baada ya miezi kulingana na utaratibu uliowekwa.

Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani (katikati mwenye kipaza sauti) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Iduda, ambao bado hawajaunganishwa na huduma ya Umeme licha ya miundombinu kuwafikia.

Hayo yameleezwa na Waziri wa Nishati ,Dkt. Medard  Kalemani , wakati wa ziara yake ya kikazi katika Jiji la Mbeya, baada ya kutembelea kituo cha  kupoza na kusambaza umeme kilichopo Mwakibete na kukagua miradi  ya kusambaza umeme katika kijiji cha Nsalaga na Iduda inayotekelezwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Alieleza kuwa, kumekuwa na changamoto ya kukatika umeme kwa muda mchache katika baadhi ya maeneo na sababu kuu ikielezwa kuwa ni hitilafu katika vituo au kuharibika kwa kifaa katika kituo cha kupoza na kusambaza umeme.

Alifafanua kuwa, changamoto hiyo inaepukika na kutoweka kabisa endapo wahandisi na mafundi watakuwa na tabia ya kufanya uchunguzi wa mitambo na mashine zao kila siku asubuhi na kubaini tatizo kabla ya kutokea.

“Mafundi na wahandisi muwe na tabia ya kufanya ukaguzi na matengenezo ya kila siku asubuhi badala ya kusubiri tatizo litokee, acheni kufanya ukaguzi na matengenezo kwa mazoea, hii itasaidia kufahamu mapema tatizo linazoweza kutokea baadaye na kuondoa usumbufu wa kukatika umeme kwa wananchi hali ya kuwa kuna umeme mwingi nawa kutosha,” alisisitiza Kalemani.

Alifafanua kuwa, kwa sasa Serikali haitaki kuona mtu yeyote anakosa huduma ya umeme kwa  sababu tu kumetokea  hitilafu katika mitambo na mashine katika vituo vya kupoza na kusambaza umeme, badala yake inataka umeme upatikane saa 24 na siku Saba kwa wiki kwa kuwa umeme upo wa kutosha na ziada.

Waziri wa Nishati, Dk.Medard Kalemani, (katikati) akipita katika mitaa ya kijiji cha Nsalaga mkoani Mbeya kukagua miundombinu ya usambazaji umeme ambapo ametoa siku 14, kwa wananchi hao kuunganishwa na huduma hiyo.

Alisema kuwa, mpango wa Serikali ni kuachana na matumizi ya majenereta kwa watu wote, wakiwemo  wafanyabiashara, Makampuni, Mashirika na pia kupunguza gharama za maisha na kurahisisha utendaji wa kazi kwa kuwa na umeme mwingi, wakutosha na ziada.

Hata hivyo,  alisema kuwa ni lazima katika kila kituo cha kupoza na kusambaza umeme kuwe na stoo ya kuhifadhi vifaa vya dharura vitakavyotumika endapo kutatokea kifaa kimeharibika au kupata hitilafu.

Alisisitiza kuwa, stoo hizo ni lazima ziwe na vifaa vizima na vya kutosha wakati wote, badala ya vifaa hivyo kuhifadhiwa katika ofisi za mameneja wa kanda au mikoa, hivyo kuleta usumbufu pindi tatizo linapotokea.

Akizungumzia huduma ya umeme wa viwandani, Dk. Kalemani alisema kuwa viwanda vikubwa vipewe umeme wa peke yao ili wazalishe kwa wingi na waweze kulipa kodi za  na kuiingizia nchi mapato.

Hivyo ametoa siku 10, kwa Tanesco, kuweka umeme wa peke yake kwenye kiwanda cha kuzalisha saruji cha Mbeya, ili kiweze kuajiri watu wengi zaidi, kuzalisha kwa wingi na kulipa kodi za Serikali.

Katika hatua nyingine, ametoa siku 14, kwa Tanesco kuhakikisha kuwa wanawaunganishia huduma ya umeme wakazi wa Kijiji cha Nsalaga na Iduda waliokidhi vigezo vya kupata huduma hiyo.

Alitolea ufafanuzi kuwa, wananchi hao waunganishiwe huduma hiyo kwa gharama ya shilingi 27,000 tu, tofauti na gharama za Tanesco kwa kuwa vijiji hivyo vipo pembezoni mwa Jiji la Mbeya, hali ya kuwa vinaoneka vipo mjini.

Akizungumzia kituo cha kuzalisha umeme cha jijini mbeya, Dk.Kalemani alisema, kituo hicho kinauwezo wa kuzalisha megawati 130, ambapo mahitaji ya Mkoa mzima wa Mbeya, Songwe pamoja na Makete ni Megawati 52, hivyo kunaziada ya megawati 78, hivyo wananchi wachangamkie fursa ya kuunganishwa na huduma ya umeme.

Na Zuena Msuya