Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameongoza kikao cha wadau mbalimbali mkoani Tanga kujadili utekelezaji wa mradi wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini unaotarajiwa kukamilika mwaka 2020.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akiwa katika kikao cha wadau wa Bomba la Mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga kilichofanyika jijini Tanga. Wa Pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, wa kwanza kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa, wa pili kushoto ni Kamishna Msaidizi wa Nishati, Mhandisi Edward Ishengoma na wa kwanza kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Zena Said.

Kikao hicho kilifanyika jijini Tanga na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, viongozi mbalimbali katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tanga, Wilaya, Halmashauri, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Wizara ya Nishati, Vyama vya Siasa, Waandishi wa Habari na baadhi  ya wananchi.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujadili hatua zinazofanyika sasa na zitakazofuata ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo ambao utapita katika mikoa Nane na wilaya 124 huku bomba likiwa na urefu wa kilometa 1444.8.

Alisema kuwa ili mradi huo ufanyike kwa ufanisi vikao kama hivyo ni muhimu kwani wadau wote wanashirikishwa na kupewa elimu kuhusu utekelezaji wa mradi, pi kupata fursa ya kujadili changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.

Katika kikao hicho, Dkt Kalemani aliwaagiza wataalam wanaohusika katika uendelezaji wa mradi huo kuhakikisha kuwa masuala yote yanayopaswa kutekelezwa ili kukamilisha mradi huo, yanafanyika kwa kasi ili mradi ukamilike ndani ya muda uliopangwa.

Katika kikao hicho, wataalam kutoka TPDC na TPA walieleza maendeleo ya utekelezaji wa mradi ikiwemo uchukuaji wa sampuli za udongo katika maeneo ambayo bomba la mafuta litapita, uwekaji wa alama za mpaka katika eneo litakalotumika kuweka miundombinu ya mafuta ghafi katika eneo la Chongoleani jijini Tanga na ununuzi wa vifaa vitakavyotumika katika Bandari wakati wa utekelezaji wa mradi ikiwemo ununuzi wa vifaa vya kunyanyua vitu vizito.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kushoto) akiwa katika eneo la Bohari ya kuhifadhi mafuta ya kampuni ya GBP jijini Tanga. Katikati ni Mkuu wa mkoa wa Tanga, Martine Shigela.

Baada ya kikao hicho cha Wadau, Dkt Kalemani alitembelea eneo la Bandari jijini Tanga na kuagiza watendaji wa Mamlaka hiyo kuhakikisha kuwa wanafunga haraka mita za kupimia mafuta (flow meters) ili Serikali ifahamu kiasi cha mafuta kinachoingia katika Bandari hiyo na kusambazwa kwa wateja.

Alisema kuwa, mita hizo zitaisaidia Serikali kujua kiwango halisi cha mafuta kinachoshushwa katika Bandari na hivyo kupata kodi stahiki.

Na Teresia Mhagama, Tanga