Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema kamwe Serikali haiwezi kumlazimisha mdau yeyote wa sekta ya mafuta nchini kujiunga na Chama, Jumuiya au Umoja wowote wa kisekta kwani hilo ni suala la hiyari kwa kila mmoja.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akizungumza na wadau wa sekta ya mafuta nchini (hawapo pichani) katika kikao kilichofanyika Februari 10, 2019 jijini Dar es Salaam. Wengine pichani, kutoka kulia ni Mwenyekiti TAOMAC, Sophonie Babo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya na Kaimu Mkurugenzi wa PBPA, Erasto Simon.

Badala yake, Waziri Kalemani, ameushauri uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Mafuta Tanzania (Tanzania Association Of Oil Marketing Companie – TAOMAC) na Jumuiya nyingine za aina hiyo, kuziimarisha zaidi kwa kuweka mazingira ambayo yatawashawishi wadau wengi kujiunga nazo.

Aliyasema hayo jana, Februari 10, 2019 jijini Dar es Salaam katika mkutano baina yake na wadau wa sekta ya mafuta nchini, wakiwemo waagizaji, wauzaji na wafanyabiashara wa mafuta.

Waziri Kalemani alikuwa akijibu ombi maalumu lililowasilishwa kwake na Mwenyekiti wa TAOMAC, Sophonie Babo na kuungwa mkono na wanachama kadhaa wa Umoja huo; kuwa Serikali iweke sheria na kanuni zitakazomlazimu mtu yeyote atakayeomba leseni ya kufanya kazi katika sekta husika kuwa kwanza mwanachama wa TAOMAC.

Akifafanua, Waziri Kalemani alisema kuwa, Serikali itaendelea na utaratibu wake wa kawaida katika kutoa leseni za biashara ya mafuta kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa ambayo hayahusishi mwombaji kuwa mwananchama wa Umoja au Jumiya yoyote ya kisekta.

“Chama ni hiari ya mtu, huwezi kumlazimisha. Kama mmeweka utaratibu mzuri, watu watajiunga tu. Hakuna sababu ya kuweka kanuni au sheria. Ukisema kuwalazimisha watu kujiunga na Chama fulani, utakuwa unaingilia uhuru wao kinyume na utaratibu wa sheria.”

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alisema malengo ya serikali ni kuhakikisha inaendelea kuisimamia sekta ya mafuta vizuri ili iweze kuwa na tija kwa pande zote mbili yaani Serikali kwa niaba ya wananchi na wafanyabishara kwa upande mwingine.

Alisema, lengo la serikali kuhakikisha sekta husika inaleta manufaa kwa wananchi wake ni la msingi na litaendelea kusimamiwa lakini pia serikali itahakikisha wafanyabiashara nao kwa upande wao wanapata faida, ilimradi walipe kodi zote stahiki.

Aidha, alisema, mifumo, será na kanuni zote zilizowekwa na serikali katika kusimamia sekta ya mafuta hazina lengo la kuathiri biashara ya mtu yeoyote bali ni kwa lengo la kusimamia maslahi ya wananchi na upande mwingine wafanyabiashara husika.

Wadau wa sekta ya mafuta, wataalamu kutoka wizarani na sekta mbalimbali za serikali, wakifuatilia kikao baina yao na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), kilichofanyika Februari 10, 2019 jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi, Mwanamani Kidaya, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Manunuzi ya Petroli kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency  – PBPA), Erasto Simon pamoja na wadau mbalimbali kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali zinazojihusisha na masuala ya mafuta.

Waziri Kalemani alielekeza kuwa kikao kama hicho kifanyike mara moja kila mwaka ili kutoa fursa kwa serikali na wadau wa sekta husika kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu uendelezaji wa sekta hiyo.

Na Veronica Simba – Dar es Salaam.