Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati wamepewa mafunzo kuhusu masuala mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia kukabiliana na changamoto za kikazi na kijamii, hivyo kuboresha utendaji wao wa kazi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. Hamisi Mwinyimvua (katikati), akifungua rasmi Semina maalum kwa wafanyakazi wa Wizara yake kuhusu masuala mbalimbali kwa lengo la kuboresha zaidi utendaji kazi. Semina hiyo imefanyika Oktoba 11, 2018 jijini Dodoma. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na RasimaliWatu, Francis Sangunaa na Kulia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Haji Janabi.

Mafunzo hayo yametolewa na wataalam mbalimbali katika semina ya siku moja iliyoandaliwa na uongozi wa Wizara, leo Oktoba 11, 2018 jijini Dodoma.

Akifungua rasmi semina hiyo, Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Hamisi Mwinyimvua, amesema uongozi unatambua kuwa wafanyakazi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kijamii na zinazohusu mahala pa kazi; lakini akawataka kushiriki semina husika kikamilifu kwa kuziweka bayana  na kutoa maoni kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzitatua.

Katika Semina hiyo, Dkt. Lyabwene Mtahabwa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma; ametoa ushauri nasaha kwa wafanyakazi waliohamia Dodoma, ambapo amewaasa kuyachukulia mabadiliko hayo kama fursa.

Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Nishati, wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa Semina maalum iliyolenga kutoa mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi. Semina hiyo imefanyika Oktoba 11, 2018 jijini Dodoma.

“Mabadiliko katika maisha ni fursa. Yatumieni mabadiliko haya kama fursa kwani kwa uzoefu wangu wa kuishi hapa kwa miaka mingi, naweza kushuhudia kuwa ni jiji lenye fursa nyingi kwa yeyote anayefungua ufahamu wake,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Mtaalam kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, Jamila Bakari, amewaasa watumishi kuzingatia suala la uadilifu katika utumishi wa umma.

Amesema kuwa, utekelezaji wa ahadi za uadilifu katika utumishi wa umma, utajenga mwitikio na dhamira ya uadilifu, uwazi, uwajibikaji, ari ya kupambana na rushwa pamoja na utoaji huduma bora katika sekta husika.

Naye Mtaalam kutoka Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dkt. Hafidhi Ameir, akitoa mafunzo ya ukimwi na magonjwa sugu yasiyoambukiza; amewaasa watumishi kuzingatia kanuni kuu nne za afya ambazo ni kuepuka msongo wa mawazo, kula chakula bora, kufanya mazoezi na kunywa maji ya kutosha.

Sehemu ya wafanyakazi wa Wizara ya Nishati, wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa wakati wa Semina maalum iliyolenga kutoa mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha utendaji kazi. Semina hiyo imefanyika Oktoba 11, 2018 jijini Dodoma.

 

Aidha, amewashauri kujenga tabia ya kununua baadhi ya vifaa vya kupima magonjwa kama sukari na shinikizo la damu, ili kujenga tabia ya kujipima wenyewe na kujitambua mapema kunapotokea viashiria vya magonjwa hayo, hali itakayowasaidia kuwaona wataalam wa afya mapema na kupata huduma stahiki, tofauti na ilivyo sasa, ambapo wengi hugundua wanaumwa wakati ugonjwa umeshakuwa mkubwa.

Watumishi pia, wamejengewa uelewa wa majukumu yao katika Wizara mpya ya Nishati ambayo ilitengwa kutoka iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini; kupitia mada iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Haji Janabi.

Vilevile, katika semina hiyo, viongozi ambao ni wakuu wa Idara na Vitengo, wameongozwa na Mtaalam kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi, kutoa ahadi za viapo kuhusu kuhusu kuzingatia maadili ya utumishi wa umma. Imeelezwa kuwa zoezi husika litafanyika kwa watumishi wengine wote mbele ya wakuu wao wa kazi.

Akifunga rasmi semina hiyo; Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na RasimaliWatu, Francis Sangunaa, amewataka watumishi kuzingatia mafunzo yote yaliyotolewa ili waweze kuboresha zaidi utendaji kazi wao.

Na Veronica Simba