Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewataka wakandarasi wote nchini wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, kuwa na Yadi maalum za kuhifadhi vifaa katika maeneo wanakotekeleza miradi hiyo, ili kuondoa kisingizio cha kutowaunganishia wananchi umeme kutokana na kutokuwepo na vifaa.

Kutoka kushoto ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Mbunge wa Nyang’hwale Hussein Kassu na Mbunge wa Igunga Seif Gulamali; wakifurahia jambo, wakati wa Mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Waziri Kalemani Chato Mjini, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi, Septemba 16, 2018.

Aliyasema hayo, Septemba 16, 2018 katika Kijiji cha Kahumo wilayani Chato, akiwa katika ziara ya kazi, ambapo pia aliwasha umeme rasmi kijijini hapo.

“Kuanzia sasa nawaelekeza muwe na Yadi zenu ambapo mtahifadhi vifaa vyote vya kazi na sisi Serikali tutazikagua. Maneneja wa TANESCO kagueni Yadi hizo.”

Waziri alitaja vifaa vya kazi vinavyotakiwa kuwepo katika Yadi hizo kuwa ni pamoja na nyaya za umeme, nguzo, transfoma pamoja na mita za Luku.

Aidha, akiwa katika Kijiji cha Magiri wilayani humo, ambako pia aliwasha umeme rasmi, Waziri Kalemani aliwaasa wananchi kuepukana na vishoka wakati wanapotaka kutandaziwa mfumo wa nyaya za umeme katika makazi yao.

Aliwataka wananchi kujiridhisha na uhalali wa mafundi watakaowatumia kuwatandazia mfumo wa nyaya, katika Ofisi za TANESCO zilizopo katika maeneo yao. Akifafanua, alisema majina ya mafundi wenye sifa yatatundikwa katika Ofisi hizo ili kuwarahisishia wananchi kuwatambua hivyo kuepukana na vishoka.

Waziri aliwahamasisha wananchi kuhakikisha wanalipia huduma ya kuunganishiwa umeme huo wa bei nafuu, ambao ni shilingi 27,000 tu ili wanufaike na Mradi husika wa Umeme Vijijini (REA), kwani Mradi huo utakapoisha, watalazimika kuunganishiwa umeme kwa bei ya kawaida, ambayo ni kubwa.

Sehemu ya umati wa wananchi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chato wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), alipowatembelea na kuzungumza nao akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Septemba 16, 2018.

Akizungumza na wananchi wa Chato Mjini katika mkutano wa hadhara, Waziri alitoa maelekezo kwa wakandarasi wa REA, kuhakikisha wanawaunganishia umeme wananchi wasiopungua 10 kwa mkupuo kila siku, tofauti na ilivyo sasa ambapo wengi wao wamekuwa wakiwaunganishia umeme wananchi wachache tu katika maeneo wanakotekeleza miradi hiyo.

“Natoa rai kwa wataalam wangu wa TANESCO na REA nchi nzima kuhakikisha wakandarasi wanaotekeleza miradi hii nchi nzima, wanawaunganishia umeme wananchi wasiopungua 10 kwa mkupuo kwa siku moja, kila tunapokwenda kuwasha umeme.”

Hata hivyo, Waziri Kalemani aliwapongeza watendaji wa TANESCO na REA kwa kazi nzuri wanayofanya ambapo alisema kuwa hali ya umeme nchini imeimarika na kwamba umeme haukatiki-katiki.

Waziri Kalemani yuko katika ziara ya kazi Kanda ya Ziwa, ambapo mbali na Mkoa wa Geita, atatembelea pia Mikoa ya Mwanza, Mara na Simiyu kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme pamoja na kuzungumza na wananchi.

Na Veronica Simba