Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani amewataka wakandarasi wanaotekeleza Mradi ya kusambaza umeme vijijini (REA III) kuacha visingizio vinavyochelewesha mradi huo kukamilika kwa wakati.

Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo wakati akizungumza wakandarasi wanaotekeleza mradi huo katika mikoa ya Mwanza na Manyara juu ya maendeleo ya utekelezaji REA III, mzunguko wa kwanza katika Mikoa hiyo.

Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani akingoza kikao hicho, kulia ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Haji Janabi.

Katika mkutano huo, Dkt. Kalemani aliwaeleza wakandarasi hao kuwa, wamekuwa na visingizio vingi kila wanapoulizwa kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika maeneo yao, na wakati mwingine visingizio hivyo havina tija.

“Wakandarasi tekelezeni mradi wa REA na ukamilike kwa wakati kama mikataba yenu inavyoelekeza, acheni visingizio visivyokuwa na tija katika utekelezaji wa mradi huo, kwa kuwa vinakwamisha shughuli za maendeleo. Unakuta mkandarasi anasingizia hana nguzo au mwingine anakwambia nyaya, lakini kiuhalisia vifaa hivyo vipo, kwakweli hii haipendezi na hakuna atakayevumilia “, alisema Dkt. Kalemani.

Kuhusu uwashaji Umeme katika vijiji, Dkt.Kalemani aliwataka wakandarasi wanaotekeleza mradi wa REA katika Mikoa ya Mwanza na Manyara kuwa kuanzia ijumaa ya wiki ijayo lazima kila kijiji kuwepo na kundi la wafanyakazi ili kuongeza ufanisi wa kazi.

Sambamba na hilo,  kila mkandarasi ahakikishe kuwa anawasha Umeme katika vijiji 3, kwa kila wiki na kwamba mameneja wanaosimamia miradi hiyo wawe mabalozi wazuri kwa wateja na kutumia lugha zisizoudhi.

Aidha, katika mkutano huo, Dkt Kalemani aliwaagiza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na TANESCO kuhakikisha kuwa kila mkoa unakuwa na mtaalam mwenye kuhakiki ubora wa  miundombinu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa REA, ikiwemo nguzo, transfoma, nyaya na vifaa vingine vinavyotumika katika mradi huo.

Vilevile, kila Mkoa uwe na vifaa vyake kwa kutathmini ubora wa miundombinu hiyo tofauti na ilivyo sasa ambapo vifaa vya kuhakiki ubora wa miundombinu vinazunguka kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine jambo linalochelewesha kazi ya kuhakiki ubora wa miundombinu hiyo.

Na Zuena Msuya

11/11/2018

windows 7 pro kaufen