Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amelitaka na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuharakisha uunganishaji wa huduma ya Gesi asilia katika nyumba za wananchi kwenye maeneo ya jiji la Dar Es Salaam kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani akizungumza na watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na watendaji wa Wizara ya Nishati, kuhusu suala la usambazaji wa Gesi asilia katika nyumba za wananchi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, ofisini kwake mkoani Dodoma

Dkt.Kalemani aliyasema hayo tarehe 3 Machi, 2018 ofisini kwake mkoani Dodoma alipokutana na watendaji wa TPDC kwa lengo la kujadili suala la usambazaji wa Gesi asilia katika nyumba za Wananchi pamoja na bei watakayouziwa wananchi hao.

Katika mazungumzo hayo, Dkt. Kalemani aliwataka TPDC kuunganisha nyumba kuanzia Hamsini (50) na kuendelea katika maeneo ya Mwenge na Mikocheni kwa kuwa tayari miundombinu ya Bomba la Gesi asilia kwa matumizi ya nyumbani limepita maeneo hayo.

kuhusu suala la bei ya kuwauzia wateja, Dkt. Kalemani alisema kuwa Gesi hiyo itauzwa kwa Wananchi kwa pungufu ya 40% ya bei ya mitungi ya gesi itakayokuwa sokoni kwa wakati huo.

“Hii ni gesi yetu na Bomba ni la kwetu, vyote vinapatikana hapahapa nchini, ni vyema iuzwe kwa bei ya chini zaidi ya ile iliyopo sokoni kwa sasa, ili kila mwananchi aweze kumudu gharama zake pia itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa na kulinda misitu yetu”, alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani pia aliwaagiza TPDC kuendelea na taratibu za kuwaunganisha wananchi wa Mtwara na huduma ya Gesi asilia katika nyumba zao kama itakavyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni.

Aidha alilishauri Shirika hilo, kutumia wataalam wake wa ndani kupitia Shirika lake Tanzu la kulinda Miundombinu ya Gesi (GASCO) ili kusambaza Gesi asilia kwenye nyumba za wananchi badala ya kutegemea wakandarasi ambao mchakato wa kuwapata unachukua muda mrefu.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Musomba (kulia) wakizungumza kuhusu suala la usambazaji wa Gesi asilia katika nyumba za wananchi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, alifafanua kuwa gharama za uunganishwaji wa huduma ya Gesi asilia katika nyumba za wananchi itategemea na ramani ya nyumba husika pamoja na umbali wa nyumba kutoka ilipopita miundombinu ya Bomba la gesi asilia linalotumika kusambaza gesi katika maeneo ya makazi.

Vilevile, Mhandisi Musomba aliweka wazi kuwa mfumo wa kusambaza Gesi asilia katika nyumba za wananchi utakuwa kama ule unaotumika kusambaza huduma ya maji, lakini ulipaji wa gharama za matumizi ya gesi hiyo utakuwa kama ule unaotumiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lipa Umeme Kadri Unavyotumia (LUKU) kwa maana kwamba kila mtumiaji atalipia huduma kadri atakavyokuwa akitumia.

Gesi itakayokuwa ikisambazwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ni ile inayozalishwa katika Visima vya Gesi vilivyopo katika Mkoa wa Lindi na Mtwara.

Na Zuena Msuya, Dodoma.