Serikali imeliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhakikisha wateja wote walime ili kuwahamasisha kuunganisha nishati hiyo katika makazi yao.

Akifafanua, Waziri alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa baadhi ya wananchi hawajaunganisha umeme katika makazi yao japokuwa tayari Serikali imekwishawafikishia nishati hiyo katika maeneo yao.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, akiwakabidhi baadhi ya wazee kifaa kinachotumika kuunganisha umeme pasipo kutandaza mfumo wa nyaya, kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) alipokuwa katika ziara ya kazi Mikoa ya Singida na Dodoma hivi karibuni.

“Inawezekana baadhi ya wananchi hawajatambua umuhimu wa kutumia umeme, hivyo ni vema wapatiwe elimu husika. Tuwatembelee mahali waliko, hususan vijijini na tuwapatie elimu hiyo,” alisisitiza.

Akizungumzia faida za umeme, Waziri Kalemani alisema umeme ni kichocheo kikubwa cha maendeleo kwani shughuli nyingi za kiuchumi zinahitaji nishati hiyo.

Aliongeza kuwa, ili dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Uchumi wa Viwanda ifanikiwe, ni lazima kuwepo na umeme wa kutosha na wa uhakika. “Ndiyo maana tumedhamiria kufikisha umeme hadi vijjijini kwa kasi kubwa, hivyo wananchi tafadhali tumieni umeme ili kukuza pato lenu na uchumi wa nchi kwa ujumla.”

Waziri aliwapongeza viongozi wa Serikali wakiwemo Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge na Watendaji wa Halmashauri na Vijiji, kwa jitihada zao za kufuatilia utekelezaji wa ahadi za serikali kwa wananchi ikiwemo upelekaji wa umeme vijijini.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutunza miundombinu ya umeme katika maeneo yao ili isihujumiwe na hivyo kuwakosesha huduma hiyo muhimu na pia kuleta hasara kwa serikali.

Afisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Innocent Lupenza, akiandika majina ya baadhi ya wazee waliopatiwa zawadi ya kifaa kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) na Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), alipokuwa katika ziara ya kazi Mikoa ya Singida na Dodoma hivi karibuni.

Ziara hiyo ya Waziri Kalemani ni muendelezo wa ziara mbalimbali ambazo amekuwa akifanya nchi nzima kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme na kuzungumza na wananchi wa maeneo husika ikiwa ni pamoja na kupokea kero na changamoto mbalimbali za wananchi kuhusu sekta ya nishati ili zifanyiwe kazi.

Katika ziara hii, Waziri ametembelea Wilaya za Mkalama na Singida Vijijini mkoani Singida pamoja na Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma.

Na Veronica Simba