Ujumbe kutoka Kampuni ya ORASCOM ya Misri, wamemtembelea Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na kuzungumza naye kuhusu nia yao ya kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe pamoja na maporomoko ya maji.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (katikati), akizungumza na Ujumbe kutoka Kampuni ya ORASCOM ya Misri (kulia), waliofika ofisini kwake Dodoma, Juni 19 2018 na kuwasilisha nia ya kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme nchini. Kushoto ni Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka.

Mazungumzo hayo yalifanyika Juni 19, 2018 Makao Makuu ya Wizara, jijini Dodoma na kuwashirikisha pia Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Tito Mwinuka.

Wakizungumzia uwezo wao katika kutekeleza nia waliyowasilisha, walieleza kuwa wana uzoefu wa miaka mingi katika kazi hiyo na kwamba wanatumia teknolojia ya kisasa. Pia, waliongeza kuwa wanazo fedha za kutosha kuweza kutekeleza miradi husika.

Aidha, waliutaja Mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe wa Kiwira wenye megawati 200 pamoja na Ruhudji wenye megawati 358, kuwa ndiyo hasa ambayo wangependa kuwekeza.

Waziri Kalemani aliyapokea mapendekezo ya Kampuni hiyo na kuwataka waendelee kufanya majadiliano na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na TANESCO kuhusu uwekezaji huo, wakati Serikali ikikamilisha utaratibu wa kuitangaza miradi husika.

Hata hivyo, Waziri alieleza bayana kuwa, Kampuni hiyo itatakiwa kushiriki katika ushindani na wawekezaji wengine wenye nia ya kuwekeza katika miradi husika, baada ya miradi hiyo kutangazwa rasmi.

Dkt. Kalemani aliishukuru Kampuni ya ORASCOM kwa kuonesha nia ya kuwekeza Tanzania na aliwahakikishia kuwa Serikali itawapa ushirikiano stahiki.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, akiagana na Ujumbe kutoka Kampuni ya ORASCOM ya Misri, waliofika ofisini kwake Dodoma, Juni 19, 2018 na kuwasilisha nia ya kuwekeza katika miradi ya umeme nchini.

Na Veronica Simba – Dodoma