Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amewaahidi wananchi katika kijiji cha Nyagh’omango wilayani Chato mkoani Geita kuwa watawashiwa umeme kabla ya tarehe 1, Januari 2018.

Hii ni  baada ya kukamilika kwa asilimia kubwa kwa taratibu za kufikisha umeme katika kijiji hicho ikiwa ni pamoja na usimikwaji wa nguzo na usambazaji wa nyaya mpaka kijijini hapo.

Nguzo za umeme katika kijiji cha Nyagh’omango wilayani Chato tayari kwa kupeleka umeme kwa wananchi.

Dkt. Kalemani aliyasema hayo tarehe 27 Desemba, 2017 wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya Umeme vijijini pamoja na kufuatilia utekelezaji wa agizo la Serikali la kuhakikisha Umeme umewekwa katika gereza la Nyagh’omango lililopo kijijini hapo kabla ya mwaka kuisha.

Akiwa katika gereza hilo, Dkt. Kalemani aliona namna mafundi wanavyotekeleza kazi ya kuweka miundombinu ya umeme kwa ufanisi ili umeme uwake ndani ya muda uliopangwa.
Akizungumza na wananchi katika kijiji hicho, aliwahamasisha kuchangamkia fursa ya kuunganisha umeme katika nyumba zao mara tu baada ya umeme kufikishwa kijijini hapo.

“Umeme ni usalama, umeme ni uchumi, umeme ndio viwanda, umeme ni kila kitu, niwaombe utakapofika kila mtu achangamkie,” alisisitiza.

“Ukiwa na nyumba yako ya ghorofa sawa, nyumba ya nyasi sawa,au ukiwa na nyumba ya tembe ni sawa, weka umeme,” aliwaasa wananchi wa Nyagh’omango kutosubiri wajenge nyumba nzuri ndipo waweze kuingiza  umeme katika nyumba zao.

Aidha, Dkt. Kalemani alitumia nafasi hiyo kuwaasa watendaji wa Tanesco, kuhakikisha kuwa wanawatumikia wananchi hasa katika kipindi cha sikukuu ya Krismasi na Mwaka mpya ili wasikose huduma za umeme, “pale ambapo wanahitaji huduma, basi Tanesco mjitoe kuwahudumia jinsi ipasavyo,” alisema Dkt Kalemani.

Kwa upande wake,  Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe alisema kuwa wilaya hiyo inapa umeme wa uhakika kwani wanapata umeme wa gridi ya taifa na kama gridi ikipata hitilafu wanapata umeme  kutoka  mtambo wa Biharamulo.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akizungumza na mafundi wanaoweka miundombinu ya umeme katika Gereza na kijiji cha Nyagh’omango wilayani Chato mkoani Geita

Aidha, amesema vijiji 74 tu ndivyo vilivyosalia katika kuunganishiwa huduma ya umeme ambapo kuna matarajio kuwa REA III itasambaza umeme katika vijiji na vitongoji ambavyo wananchi wengi wanaomba huduma hiyo ya umeme.