Katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini (Awamu ya Tatu) unatekelezwa kwa ufanisi, wataalam kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati wamefanya kikao na Wakandarasi waliopewa kazi ya kusambaza umeme Vijijini katika Mkoa wa Mtwara kupitia Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III).

Vikao hivyo ambavyo ni endelevu, vinalenga katika kupata taarifa sahihi za utekelezaji wa miradi hiyo kutoka kwa Wakandarasi na pia kujadili changamoto ili kuzitafutia ufumbuzi lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa miradi hiyo inafanyika kwa ufanisi kama ambavyo Mkataba kati ya Serikali na Wakandarasi hao unaelekeza.

Aidha, pamoja na kufanya vikao na Wakandarasi hao, Wasimamizi wa Mradi huo kutoka Wizara na Taasisi wamekuwa wakitembelea katika maeneo ambayo kazi ya usambazaji umeme vijijini inaendelea kwa lengo la kujiridhisha kama miradi hiyo inafanyika kwa ufanisi.

Mhandisi Fadhili Chilombe, kutoka TANESCO, anayesimamia mradi wa REA III katika Mkoa wa Mtwara (wa Saba kutoka kulia) akiongoza kikao kilichohudhuriwa na Wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini Mkoa wa Mtwara, Mameneja wa TANESCO wa Wilaya katika Mkoa wa Mtwara na Mhandisi Styden Rwebangila, kutoka Wizara ya Nishati anayesimamia Mradi wa REA III katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, (wa kwanza kushoto).

Kikao kilichofanyika tarehe 22 Mei, 2018, mjini Mtwara, ambacho Mwenyekiti wake alikuwa Fadhili Chilombe, Mhandisi kutoka TANESCO anayesimamia mradi wa REA III katika Mkoa wa Mtwara, kilihudhuriwa pia na Mameneja wa TANESCO kutoka Wilaya za Mkoa wa Mtwara,  Mhandisi Styden Rwebangila, kutoka Wizara ya Nishati anayesimamia Mradi wa REA III katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma na wakandarasi wanaosambaza umeme katika mkoa wa Mtwara.

Katika Kikao hicho, Mhandisi Chilombe pamoja na kuwataka wakandarasi kufuata muongozo wa utendaji kazi uliotolewa na Serikali, alisema kuwa tofauti na ilivyokuwa hapo awali, kwa sasa kuna ushirikiano mkubwa kati ya Wakandarasi hao pamoja wasimamizi wa Mradi kutoka Wizara na Taasisi hali inayopelekea kila upande kuwa na taarifa sahihi ya utekelezaji wa mradi.

Aidha, alipongeza uamuzi wa Waziri wa Nishati wa kuamua kuteua Wataalam kutoka Wizara ya Nishati wanaosimamia mradi huo katika kila kanda suala linalopelekea Viongozi wa Wizara kupata taarifa sahihi ndani ya muda mfupi kuhusu hatua za utekelezaji wa mradi.

Na Mwandishi Wetu, Mtwara