Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wakiongozwa na Mhandisi Yusuph Msembele kutoka Wizara ya Nishati, wamekagua mradi wa umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III) katika wilaya mbalimbali mkoani Tanga na kuzindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Bagamoyo, wilayani Korogwe.

Mhandisi Yusuph Msembele kutoka Wizara ya Nishati (wa Tatu kulia) akikata utepe kuashiria kuanza kupatikana kwa huduma ya umeme katika Kijiji cha Bagamoyo wilayani Korogwe mkoa wa Tanga. Wengine katika picha ni Wataalam kutoka TANESCO, REA na wawakilishi wa wananchi.

Mhandisi Msembele, ambaye alimwakilisha Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu katika uzinduzi huo, alisema kuwa, kuzinduliwa kwa huduma ya umeme katika Kijiji hicho kumewezesha wananchi zaidi ya 63 kuunganishwa na huduma ya umeme huku wateja 180 tayari wameshalipia huduma hiyo.

” Niwapongeze wananchi wa Kijiji hiki cha Bagamoyo kwa kuchangamkia huduma ya umeme, lakini niwakumbushe kuwa inapaswa kutumia umeme kwa ajili ya kufanya shughuli za kiuchumi kama kufunga mashine za kusaga nafaka na si kuwasha taa peke yake, ” alisema Mhandisi Msembele.

Wataalam wengine walioambatana na Mhandisi Msembele ni  Afisa Upimaji kutoka REA, Hussein Shamdas, Meneja wa TANESCO mkoa wa Tanga,  Eng. Cecilia  Msangi na Meneja wa TANESCO, wilaya ya Korogwe, Julius Nyamarungu.

Aidha, wataalam hao walikagua kazi ya usambazaji umeme vijijini katika Kijiji cha Magila-Gereza wilayani Korogwe ambapo Mkandarasi kutoka kampuni ya Derm Electrics, alisema kuwa, umeme katika Kijiji hicho utawashwa baada ya Wiki Moja kwani kazi mbalimbali zimekamilika ikiwemo kuweka nguzo na kwamba, wateja 50 wanatarajiwa kuunganishwa na huduma ya umeme.

Vilevile, Wataalam hao walikagua kazi ya usambazaji umeme vijijini katika Kijiji cha Nkelei wilayani Lushoto ambapo Mkandarasi, Kampuni ya Derm Electrics, alisema kuwa atawasha umeme katika Kijiji hicho baada ya Wiki Mbili.

Wataalam kutoka Wizara ya Nishati, REA na TANESCO wakikagua kazi ya usambazaji umeme vijijini katika Kijiji cha Magila-Gereza wilayani Korogwe. Wa kwanza kushoto ni Mhandisi Yusuph Msembele kutoka Wizara ya Nishati aliyemwakilisha Naibu Waziri wa Nishati katika ziara hiyo.

Wataalam hao, kwa nyakati tofauti waliwaeleza wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya umeme ili kusiwe na changamoto ya upatikanaji wa nishati husika na wananchi kutokutoa rushwa ili kuunganishwa na huduma ya umeme kwani gharama ya kuunganisha huduma hiyo wakati wa utekelezaji wa mradi ni shilingi 27,000.