Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji Nchini (Ewura)  na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia upya bei za umeme na kuwasilisha mapendekezo ya bei mpya ifikapo Agosi 15 ili kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha na kuongeza wateja wa umeme wa Tanesco.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco Dkt. Tito Mwinuka akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu wakati wa kikao kazi kilihofanyika baina ya wizara na taasi zake mwanzoni mwa mwezi Agosti, 2018

Aidha amemwagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco nchini Alexander Kyaruzi kuwachukulia hatua mameneja wa kanda, mikoa na wilaya wa Tanesco watakashindwa kusimamia zoezi la kuwaunganishia wananchi umeme ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo iliyojiwekea ya kuifanya nchi kuwa na uchumi wa viwanda.

Maagizo hayo yametolewa jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua kikao cha kazi kilichowakutanisha watendaji na wajumbe wa bodi wa Tanesco, Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Ewura pamoja na watendaji kutoka Wizara ya Nishati kilichofanyika tarehe 5 mwezi Agosti, 2018 katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa.

Akizungumzia umuhimu wa kikao hicho, Dkt Kalemani alisema kimelenga katika kujadili mapungufu, changamoto, na mafanikio  ya utendaji kazi za kila siku za wajumbe hao ili kuwezesha kutatua masuala yanayochelewesha utekelezaji wa majukumu, kupongeza na kufikia muafaka wa namna ya kutekeleza majukumu yao kwa pamoja.

Aidha, Kalemani amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kupunguza kero za kukatikakatika kwa umeme nchini na hasa katika mikoa ya kusini yaani Lindi na Mtwara na kwamba wananchi hawajapleka malalamiko na badala yake  wanapongeza kwa kazi inayofanyika.

Akizungumzia suala la kuwasha umeme vijijini, Dkt. Kalemani amewataka REA ambao ni wasimamizi wakuu wa mradi, kuhakikisha wakandarasi wanawasha umeme katika vijiji vitatu kwa wiki ili kwenda na kasi na kukamilisha mradi kwa wakati.

“Wizara yetu inakazi kubwa ya kuhakikisha nchi inaingia katika nchi yenye uchumi wa kati kupitia uchumi wa viwanda, Uchumi wa viwanda hauwezekani kusipokuwepo na nishati ya umeme, hivyo hakikisheni umeme wa REA unaunganishwa na kusababisha matokeo chanya ya kuwa na viwanda vingi ili kusaidia nchi kujiongezea kipato kutokana na mapato yatakayotokana na uzalishwaji wa viwandani”. Alisisitiza.

Aidha, aliwasisitizia Tanesco kusimamia matumizi ya mapato yanayokusanywa na shirika hilo, alisema makusanyo yameongezeka lakini anashangazwa kuona kuwa jinsi makusanyo yanavyopaa na matumizi ya mapato hayo yanaongezeka hivyo. “Makusanyo yakiongezeka na matumizi ni hasara, hapo lazma kuna tatizo”. Alisema.

Dkt. Kalemani alizungumzia suala la ununuzi wa vipuli vya kuwaunganishia umeme wateja na kuliagiza shirika la Umeme nchini kuzipa uwezo ofisi za kanda ili kununua vifaa hivyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwepo na stoo za kutunza vifaa hivyo katika ofisi za kanda, mikoa na wilaya ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu kuliko kutegemea manunuzi kufanywa na ofisi ya makao makuu ya shirika peke yake.

Aidha, alibainisha kuwa, ipo miradi ya kuzalisha umeme lakini bado inasuasua, wanaohusika na utekelezaji wa miradi hiyo wafanye haraka kuitekeleza bila kusua sua.

Akizungumzia suala la kubadilisha mita za zamani na kuweka mita za luku, Kalemani amewataka wahusika kuhakikisha ifikapo Agosti 30 mita zote za zamani ziwe zimebadilishwa.

Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Nishati Haji Janabi akizungumza jambo kabla ya ufunguzi rasmi wa kikao kazi cha wizara na taasisi zake mwanzoni mwa mwezi Agosti.

Akizungumzia matarajio na matokeo ya kikao hicho, Dkt. Kalemani amewataka watendaji wote baada ya kikao kwenda kuimarisha maeneo yao ya kazi. “Tukitoka katika kikao hiki twende tukaimarishe maeneo yetu, hatutasita kukuchukuia hatua ukifanya tofauti na makubaliano, lazima tujiamini tufanye kazi kwa ufanisi na kwa haraka. Tuweke mikakati maeneo yote ambayo hayajawashwa umeme yawashwe”. Alisisitiza.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa REA Amos Maganga amesema, wakala umejipanga kikamilifu kuhakikisha kuwa umeme unafika katika vijiji vyote nchini kama ilivyokusudiwa ili umeme uweze kuleta mchango wake kaika kukuza uchumi wa nchi.

Aidha, Maganga alizungumzia lengo la wakala la kuongeza vijiji 1542 kwenye miradi ya kusambaza umeme awamu ya tatu ambavyo kwa namna moja au nyingine havikuwemo katika mpango wa awali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura kwa upande wake alisema, agizo la kushusha bei ya umeme kama lilivyotolewa na Waziri wa Nishati limepokelewa na wameshaanza kulifanyia kazi hivyo wako katika hatua ya kuliwakilisha kwenye bodi ya Ewura ili waweze kupewa mwongozo.

Na. Nuru Mwasampeta, Dodoma