Waziri Kalemani aagiza vituo vyote vya kuzalisha umeme nchini vihifadhi vifaa vya ziada

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameuagiza uongozi wa Shirika la Umeme Tanzania kuhakikisha vituo vyote vya kuzalisha na kupoozea umeme nchi nzima vinakuwa na hifadhi ya vifaa vya ziada zikiwemo transfoma.

Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (kulia), akitoa maagizo kwa Msimamizi wa Kituo cha kupooza umeme cha Kaale, kilichopo Tabora Mjini, Mhandisi Noel Kaale wakati alipotembelea kituo hicho akiwa katika ziara ya kazi mkoani Tabora, Desemba 14, 2018.

Alitoa agizo hilo, Desemba 14, 2018 mkoani Tabora, alipotembelea kituo cha kupoozea umeme cha Kiloleni kilichopo Tabora Mjini.

Akifafanua kuhusu agizo hilo, Waziri Kalemani alisema kuwa lengo la kuwa na hifadhi hiyo ya vifaa muhimu ni kwa ajili ya kuwezesha kubadilisha vifaa vibovu mara moja pale inapotokea kifaa kimeharibika hivyo kituo kuendelea kufanya kazi kama kawaida, badala ya kutumia muda mrefu kuagiza na kuwasumbua wananchi kwa kuwakosesha huduma ya umeme.

Aidha, Waziri Kalemani aliwaagiza mameneja na wasimamizi wa vituo hivyo nchi nzima, kuhakikisha wanafanya ukaguzi na marekebisho ya mitambo katika vituo hivyo kila siku.

“Najua ninyi ni wataalamu na mnafanya ukaguzi wa mitambo husika kila mara, lakini nami nasisitiza mfanye ukaguzi huo kila siku ili kuhakikisha muda wote iko katika hali nzuri.”

Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Tabora, Mhandisi Seraphine Lyimo, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi yake kwa Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (meza kuu), alipokuwa katika ziara ya kazi mkoani humo, Desemba 14, 2018 kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme na kuzungumza na wananchi.

Akitolea ufafanuzi wa suala hilo, Waziri alisema kuwa “hata magari, kila unapofanya ukaguzi wake unaambiwa ukaguzi unaofuata ni baada ya kilomita kadhaa; lakini haikuzuii kila siku kukagua maji, vilainishi na kadhalika.”

Pia, alisisitiza kuwa hatapenda kusikia kero ya umeme kwa Mkoa wa Tabora kwani umeme uliopo ni mwingi kuzidi mahitaji.

Awali, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa kituo hicho, Msimamizi wake, Mhandisi Noel Kaale alimweleza Waziri na Ujumbe aliofuatana nao kuwa, kituo husika kinaweza kubeba megawati 40.5 za umeme ilhali matumizi ya Mkoa mzima hayazidi nusu ya uwezo wa kituo hicho.

Katika ziara hiyo, Waziri Kalemani alifuatana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gift Msuya, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Almasi Maige, viongozi na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani, TANESCO, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Chama Tawala CCM.

Na Veronica Simba

 

microsoft project 2016 kaufen