Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani leo tarehe 07 Juni, 2018 amefanya ziara katika kata za Nyamirembe na Nyambiti zilizopo wilayani Chato mkoani Geita, lengo likiwa ni kukagua kazi ya usambazaji wa miundombinu ya umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) pamoja na kuzungumza na wananchi.

Kutoka kushoto, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Raymond Seya, Mkurugenzi Ufundi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Bengiel Msofe wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)

Katika ziara yake Waziri Kalemani aliambatatana na wataalam kutoka Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO). Akizungumza na wananchi katika nyakati tofauti, Dkt. Kalemani alielekeza mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha vijiji pamoja na vitongoji vyake vyote vinapata umeme na kuhakikisha kazi inakamilika katika muda uliopangwa.

Aidha, Dkt. Kalemani aliwataka wananchi kujiandaa na uunganishwaji wa huduma ya umeme kwa kutandaza mifumo ya umeme (wiring ) kwenye nyumba zao na kusisitiza kuwa gharama ya kuunganishwa na huduma ya umeme ni shilingi 27,000 tu.

Sehemu ya wakazi wa Kata ya Nyamirembe iliyopo wilayani Chato mkoani Geita wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) katika mkutano wa hadhara.