Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amekutana na Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kuipa changamoto kuhakikisha shirika hilo linajiendesha kibiashara.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Profesa Sufian Bukurura (kushoto), akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wa pili-kulia) na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika hilo (hawapo pichani), kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Shirika hilo jijini Dar es Salaam, jana Februari 10, 2019. Wengine pichani ni Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia) na Katibu Mkuu Dkt. Hamisi Mwinyimvua (wa pili-kushoto).

Alitoa changamoto hiyo jana Februari 10, 2019 jijini Dar es Salaam, ambapo aliwaelekeza wajumbe wa Bodi husika kuandaa andiko mahsusi likieleza namna shirika hilo linavyoweza kujiendesha kibiashara na kuleta tija zaidi kwa Taifa na wananchi pasipo kutegemea ruzuku kutoka serikalini.

Kikao hicho pia kiliwashirikisha Naibu Waziri wa Nishati Subira Mgalu, Katibu Mkuu, Dkt. Hamisi Mwinyimvua na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, Raphael Nombo; ambapo mambo mbalimbali yahusuyo utendaji wa shirika yalijadiliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba (kushoto), akizungumza wakati wa kikao cha Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo (hawapo pichani), kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi za Shirika hilo jijini Dar es Salaam, jana Februari 10, 2019.

Na Veronica Simba – Dar es Salaam.