Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, amewaagiza Mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Wilaya na Mikoa yote nchini, kushughulikia changamoto ya kukatikakatika kwa umeme, ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Uongozi wa Wizara ya Nishati wakiwa katika kikao cha kazi na Wenyeviti wa Bodi za TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Menejimenti za REA na TANESCO, Mameneja wa Kanda, Mikoa na Wilaya wa TANESCO, pamoja na Wafanyakazi wa Wizara. Kikao hicho kilichofanyika Juni 24, 2018 katika ukumbi wa Hazina, Dodoma.

Alitoa maagizo hayo jana, Juni 24, 2018 wakati wa kikao cha kazi baina yake na Wenyeviti wa Bodi za TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Menejimenti za REA na TANESCO, Mameneja wa Kanda, Mikoa na Wilaya wa TANESCO, pamoja na Wafanyakazi wa Wizara ya Nishati, kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina, Dodoma.

Dkt. Kalemani alisema kuwa, kero inayosumbua zaidi wananchi ni kukatikakatika kwa umeme, hivyo ni lazima ishughulikiwe kikamilifu na kuitatua mapema iwezekanavyo.

“Naagiza kila Meneja afuatilie chanzo cha kukatika kwa umeme katika eneo lake na kulishughulikia ndani ya mwezi mmoja. Hadi kufikia Julai mwishoni, tuwe tumerekebisha.”

Aidha, Waziri aliwaagiza watendaji hao kuhakikisha wanaendelea na zoezi la kuwaunganishia wateja umeme nchi nzima huku wakizingatia kanuni zinazowezesha ufanisi wa kazi ambazo ni kasi, nidhamu na usahihi.

Vilevile, aliwataka kufanyia kazi kwa haraka masuala ya ulipaji fidia wananchi ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya umeme nchini kote.

Pia, Waziri alisisitiza suala la ubunifu, hususani katika utoaji huduma kwa wananchi. “Mathalani, yako maeneo ambayo mahitaji ya umeme kwa wananchi ni makubwa lakini hakuna ofisi za TANESCO. Maeneo kama hayo hayapaswi kusubiri uwepo wa Jengo la Ofisi ndipo yapelekewe huduma. Ofisi siyo Jengo bali ni huduma. Hivyo, tuandae utaratibu wa kupeleka huduma katika maeneo hayo.”

Pamoja na changamoto hizo, Waziri alikiri kuwa utendaji wa TANESCO umekuwa ni wenye kuridhisha kwa kiasi kikubwa na hivyo aliwapongeza watendaji wake wote na kuwataka waendelee kuboresha zaidi utendaji wao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, pamoja na kuungana na Waziri katika kupongeza utendaji wa TANESCO; aliwataka watendaji hao kuiga mbinu kutoka kwa wale wanaofanya kazi vizuri zaidi ili kuendelea kuboresha huduma wanazotoa kwa wananchi.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Nishati, Lusius Mwenda (mbele), akiwa katika kikao cha kazi baina ya Uongozi wa Wizara (hawapo pichani) na Wenyeviti wa Bodi za TANESCO na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Menejimenti za REA na TANESCO, Mameneja wa Kanda, Mikoa na Wilaya wa TANESCO, pamoja na Wafanyakazi wa Wizara, kilichofanyika Juni 24, 2018 katika ukumbi wa Hazina, Dodoma.

Wakizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wote, kwa nyakati tofauti, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Mhandisi Salum Inegeja, Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Alexender Kyaruzi pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Dkt. Gideon Kaunda, waliahidi kuwa, watatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na viongozi hao ili kuleta ufanisi zaidi katika utendaji wa sekta ya nishati.

Katika kikao hicho cha kazi, wajumbe mbalimbali walipata pia fursa ya kuwasilisha changamoto na maoni yao kuhusu utendaji kazi, ambazo zilijadiliwa na mwishoni kutolewa mwongozo na Waziri.

Na Veronica Simba – Dodoma.