• Uzinduzi waenda sambamba na upatikanaji maji kutoka Mtambo mpya

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi huduma ya umeme katika Kata ya Kigwe iliyopo wilayani Bahi, Mkoa wa Dodoma.

Uzinduzi huo uliofanyika mwishoni mwa Juma, Jumamosi Februari 10 mwaka huu, ulienda sambamba na ufunguzi wa Mtambo wa Maji ambao umeweza kufanya kazi kutokana na upatikanaji wa huduma hiyo ya umeme.

Kutoka kushoto ni Mbunge wa Bahi Omari Baduel, Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na Mkuu wa Wilaya ya Bahi Elizabeth Kitundu wakati wa ziara ya Waziri Kalemani kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme wilayani humo Februari 10 mwaka huu.

Waziri Kalemani alifanya uzinduzi huo akiwa katika ziara ya kazi wilayani Bahi kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa wilayani humo.

Awali, akiwa katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge kumweleza nia ya ziara yake, Waziri alisema kuwa wananchi zaidi ya 200 wataanza kupata umeme kufuatia tukio la kurasimishwa kuwashwa kwa nishati hiyo Kigwe.

“Tunatoa kipaumbele sana kwa Mkoa wa Dodoma kwa sasa kwani ni Makao Makuu. Tunaweka juhudi za makusudi kuhakikisha kwamba wananchi wengi wanapata umeme na huduma hiyo inakuwa ya uhakika,” alisema Dkt. Kalemani.

Akifafanua zaidi, alisema kuwa, Serikali imeanzisha harakati za kufanya ukaguzi kwenye utekelezaji wa Miradi yote ya umeme mkoani humo.

Alieleza kuwa lengo la kufanya hivyo siyo tu kwa sababu Dodoma ni Makao Makuu bali pia kama Mkoa, imebainika kuwa miundombinu yake katika baadhi ya maeneo imepoteza ubora, hasa nguzo. Hii ni kwa sababu eneo hili ni tambarare na hivyo mvua ikinyesha maji yanatuama na kuharibu nguzo mara kwa mara.

“Kwa hiyo tunaendelea na ukaguzi wa miundombinu ili kuhakikisha Dodoma inaendelea kupata umeme wa uhakika muda wote.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa pamoja na kupongeza jitihada ambazo Wizara ya nishati imekuwa ikifanya nchi nzima katika kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana katika maeneo mbalimbali, pia alimwomba Waziri Kalemani kuupa upendeleo Mkoa huo kwa kuwa ni kitovu cha nchi.

Akiwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bahi katika ziara yake, Waziri Kalemani aliwasisitiza wananchi kufanya maandalizi ili umeme utakapounganishwa katika maeneo yao waweze pia kuunganisha katika makazi yao na katika maeneo yao mbalimbali ya kazi.

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwataka viongozi wa Halmashauri mbalimbali za vijiji kote nchini, kuhakikisha wanajiandaa kwa ajili ya kuunganishiwa umeme katika taasisi zote za umma zikiwemo Shule, Vituo vya Afya, Miradi ya Maji, Masoko na nyinginezo.

Vilevile, alikumbushia umuhimu wa kila mmoja kuhakikisha baada ya kuunganishiwa umeme katika eneo lake anakumbuka kulipa bili za huduma hiyo muhimu.

“Usipolipa, Serikali itakukatia umeme hivyo kurudisha nyuma maendeleo yako,” alisisitiza.

Jambo jingine ambalo Waziri Kalemani alisisitiza ni kwa wakandarasi kuhakikisha wanawagawia bure wateja 200 wa kwanza watakaojitokeza kuunganishiwa umeme wa REA, kifaa cha Umeme Tayari (UMETA) kama ilivyoelekezwa na Serikali na siyo vinginevyo.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (mwenye suti ya bluu) na Mbunge wa Bahi Omari Baduel, wakiwatwika ndoo za maji wananchi wa Kijiji cha Kigwe wilayani Bahi, baada ya kuzindua huduma ya umeme uliowezesha Mtambo mpya wa Maji kufanya kazi na kuanza kutoa huduma kwa wananchi. Uzinduzi ulifanyika Februari 10 mwaka huu.

“Kifaa hicho hakiuzwi kwa sasa hadi wateja 200 wa mwanzo wakamilike na kugawiwa bure ikiwa ni njia ya kuhamasisha wananchi wengi vijijini kujitokeza kuunganisha umeme. Mkandarasi yeyote atakayebainika kuwauzia wananchi au kutowapatia kifaa hicho wale wateja 200 wa kwanza kama tulivyoelekeza, tutamchukulia hatua.”

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Elizabeth Kitundu na Mbunge wa Jimbo hilo, Omari Baduel walipongeza jitihada za Serikali kupitia Wizara ya Nishati katika kuhakikisha wananchi, hususan wa vijijini wanafikiwa na huduma muhimu ya umeme.

Akiwasilisha taarifa ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwa Waziri Kalemani katika ziara hiyo, Meneja wa Shirika hilo wa Wilaya ya Bahi, Kitila Bryceson alisema kuwa, Wilaya hiyo ina jumla ya wateja 1498 wa umeme hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu na kwamba ina laini ya umeme yenye urefu wa jumla ya kilomita 78.8 na jumla ya Mashine Poozo (Transfoma) 35 zinazohudumia wananchi, taasisi na viwanda.

Na Veronica Simba – Dodoma