• Azindua mradi wa upanuzi wa Kituo cha Umeme na uingizaji wa mafuta katika Bandari ya Mtwara 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa, tarehe 21 Mei, 2018 amezindua miradi ya nishati mkoani Mtwara itakayopelekea Mkoa huo pamoja na Lindi kupata umeme wa uhakika pamoja na kununua mafuta kwa bei sawa na Dar es Salaam.

Mitambo mipya ya umeme (MW 4) iliyofungwa katika Kituo cha kuzalisha umeme cha Mtwara.

Mradi wa kwanza aliouzindua ni upanuzi wa kituo cha kufua umeme cha Mtwara ambacho kimefungwa mitambo mipya ya megawati 4 ambayo itasaidia kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme katika mikoa hiyo kutokana na upungufu wa uzalishaji umeme uliokuwepo katika kituo cha kufua umeme wa Gesi Asilia cha Mtwara.

Kituo cha kufua umeme wa Gesi Asilia cha Mtwara kina uwezo wa kuzalisha megawati 18 lakini uwezo wa sasa ni megawati 15.8 kufuatia kuharibika kwa mtambo namba 9 ambapo kandarasi ya matengenezo yake imeshakabidhiwa kwa kampuni ya Mantrac na ukarabati wa mtambo huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi wa Tisa, mwaka huu.

Waziri Mkuu pia alizindua mradi wa kuingiza mafuta katika Bandari ya Mtwara kufuatia agizo alilolitoa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli mwezi Machi mwaka jana la kutaka uagizaji wa mafuta kwa mikoa ya Kusini ufanyike kupitia Bandari ya Mtwara.

Awali, Bandari hiyo ilikuwa ikipitisha mafuta kwa ajili ya watumiaji katika miradi mbalimbali mkoani Mtwara na si wananchi, lakini sasa mafuta yataanza kupakuliwa kwa ajili ya wananchi ambap

o kuanzia mwezi Juni mwaka huu tani 10,000 za mafuta zitaanza kushushwa zikiwemo tani 7000 za mafuta ya dizeli na tani 3000 za mafuta ya petroli.

Akizungumza na wananchi mkoani Mtwara, Waziri Mkuu, alisema kuwa, Serikali inaendelea na jitihada za usambazaji umeme nchini ambapo kwa sasa  maeneo ya mjini yanayofanana na vijiji nayo yatapelekewa umeme kwa gharama zinazotumika katika mradi wa usambazaji umeme vijijini ambayo ni 27,000.

Alisema  kuwa, kufungwa mitambo mipya ya umeme mkoani Mtwara kutatatua changamoto iliyokuwepo hapo awali ya ukatikaji wa umeme mara kwa mara katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kuhusu uingizaji wa mafuta kupitia Bandari ya Mtwara, alizipongeza kampuni za Oilcom na GM kwa kuamua kuyafufua matenki mawili ya kupokea mafuta yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni ishirini na Sita.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa akikagua miundombinu katika Bandari ya Mtwara ambayo itawezesha Bandari hiyo kuanza kupakua mafuta kuanzia mwezi Juni mwaka huu. Kulia kwake ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.

Alisema kuwa, Serikali imeshakarabati mitambo ya kupokelea mafuta katika Bandari hiyo pamoja na kujenga mabomba yatakayopeleka mafuta katika matenki hayo  suala linalopelekea Bandari hiyo kuanza kupokea Meli kubwa zilizosimama kutoka mwaka 2014 ili kushusha mafuta yatakayosafirishwa hadi nje ya nchi.

Aidha, aliitaka Mamlaka ya Bandari Tanzania kuacha urasimu katika utendaji kazi, kutumia lugha nzuri na kuwatia hamasa watumishi ili Bandari hiyo ifanye kazi kwa ufanisi na hivyo kuvutia watu binafsi na kampuni mbalimbali kutumia Bandari hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani, alisema kuwa kutumika kwa Bandari ya Mtwara kupokea mafuta, kutasaidia kuinua uchumi wa Mkoa wa Mtwara, kuongeza ufanisi katika kupokea mafuta nchini na kupata sehemu nyingine ya kupakulia mafuta baada ya Dar es Salaam na Tanga.

Na Teresia Mhagama, Mtwara.